HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA TISA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 23 APRILI 2010, DODOMA
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumaliza shughuli zote zilizopangwa katika Mkutano huu wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania salama.
2. Mheshimiwa Spika, tanguMkutano wa 18 wa Bunge, Nchi yetu imeendelea kukumbwa na majanga mbalimbali yakiwemo mafuriko katika maeneo mbalimbali Nchini. Vilevile kumekuwepo na ajali ya kufukiwa na kifusi cha Udongo katika Mgodi ulioko Wilayani Geita Mkoani Mwanza iliyotokea tarehe 12 Aprili 2010. Katika ajali hiyo Watu 8 walifariki na wengine kujeruhiwa. Aidha, majanga mengine ni Ajali za Majini ambapo watu walikufa Maji na pia wapo wengi waliopoteza maisha kwa ajali za Barabarani. Napenda kuwapa pole waliopoteza ndugu zao katika ajali hizi. Tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu Mahala Pema Peponi. Amina.
SHUGHULI ZA BUNGE
a) Maswali
3. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Kumi na Tisa wa Bunge, jumla ya Maswali 118 ya Msingi na 249 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Wizara husika. Aidha, Utaratibu wa Maswali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kila Alhamisi uliendelea kwa Waheshimiwa Wabunge kuuliza na kujibiwa maswali yao. Jumla ya Maswali 18 ya Msingi na 5 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kikamilifu.
b) Miswada
4. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, jumla ya Miswada Nane (8) imesomwa na kupitia hatua zake zote. Miswada hiyo ni:
i) Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2010 [The Persons With Disabilities Bill, 2010];
ii) Muswada wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo wa Mwaka 2010 [The Livestock Identification, Registration and Traceability System Bill, 2010];
iii) Muswada wa Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo wa Mwaka 2010 [The Grazing-Land and Animal Feed Resources Bill, 2010];
iv) Muswada wa Sheria wa Kurekebisha Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2010 [The Financial Laws (Miscellaneous Ammendments) Bill, 2010];
v) Muswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana wa Mwaka 2010 [The Capital Markets and Securities (Ammendments) Bill, 2010];
vi) Muswada wa Sheria ya Madini wa Mwaka 2010 (The Mining Bill, 2010);
vii) Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2010 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2010];
c) Maazimio
5. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilijadili na kupitisha Maazimio mawili ambayo ni:
i) Azimio la Kuongeza Mtaji wa Mfuko wa Dhamana (Advance Fund); na
ii) Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki.
d) Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge
6. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, pia Bunge lako Tukufu lilipokea na kujadili Taarifa za Kamati mbalimbali za Kudumu za Bunge kama ifuatavyo:
i) Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Local Authorities Accounts Committee - LAAC);
ii) Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee – PAC);
iii) Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Parastatal Organisation Accounts Committee – POAC).
e) Kauli za Mawaziri
7. Mwisho, Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli ya Waziri wa Habari na Utamaduni na Michezo kuhusu matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi za Serikali na Kauli ya Waziri wa Miundombinu kuhusu uharibifu wa Miundombinu ya Barabara na Reli Nchini.
8. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri mliyoifanya katika kujadili na kupitisha Miswada, Maazimio na Taarifa za Kamati mbalimbali zilizowasilishwa hapa Bungeni. Aidha, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri mlioutoa ambao utasaidia katika utekelezaji wa Sheria na Maazimio yaliyopitishwa.
KILIMO:
Mkutano wa Watafiti wa Sekta ya Kilimo
9. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali za kutoa msukumo katika Kilimo na pia kukabiliana na changamoto zake, tarehe 17 na 18 Machi 2010 ulifanyika Mkutano wa pamoja wa Watafiti wa Sekta ya Kilimo, kwa maana ya Utafiti wa Mazao, Mifugo na Uvuvi, Jijini Dar es Salaam. Mkutano huu, ulilenga katika kupata Taarifa za hali ya tafiti zinazoendelea kwenye Vituo mbalimbali hapa Nchini pamoja na Changamoto zinazowakabili Watafiti.
10. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huo, Watafiti walipata fursa ya kueleza namna wanavyofanya kazi zao pamoja na mafanikio ya ugunduzi wa Teknolojia zinazosaidia katika kuendeleza Sekta ya Kilimo. Hii ikiwa ni pamoja na ugunduzi wa Mbegu Bora, Urutubishaji Udongo, Pembejeo, Kilimo cha Umwagiliaji na Ushauri wa Kitaalam kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
11. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa Watafiti pia ulijadili na kuainisha. Changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji wa kazi kwenye Vituo vyao vya Utafiti, Changamoto hizi ni pamoja na:
(a) Ufinyu wa Bajeti ya Utafiti;
(b) Upungufu wa Wataalam na maslahi duni ya Watafiti;
(c) Ukosefu wa Miundombinu na Vitendea kazi kwa Watafiti: Hii ni pamoja na ukosefu wa Maabara za kisasa, Ofisi, Nyumba za kuishi Watafiti pamoja na maghala ya kutunzia bidhaa.
(d) Ukosefu wa Zana za Kilimo na Pembejeo za kufanyia kazi, hususan Matrekta, Magari, Pikipiki na Baiskeli.
(e) Usambazaji hafifu wa Teknolojia, zinazogunduliwa na Watafiti. Hii imesababisha mawasiliano duni kati ya Mtafiti, Mgani na Mkulima na kusababisha Teknolojia zinazogunduliwa kutowafikia walengwa.
(f) Vituo vya Utafiti kutokuwa na Hati za kumiliki Ardhi: Hivi sasa, Maeneo mengi ya Vituo vya Utafiti yamevamiwa na Watumiaji wengine wa Ardhi, hasa kutokana na ukweli kuwa Vituo vya Serikali havijapimwa na hii inatokea hasa kwenye maeneo ya Vituo vilivyo karibu na miji inayoendelea kupanuka.
12. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na Changamoto zilizobainishwa na Watafiti, Serikali itachukua hatua zifuatazo:
(a) Bajeti ya Utafiti itaongezwa kuanzia Mwaka ujao wa Fedha kwa lengo la kufika/kukaribia Asilimia moja ya Pato la Taifa;
(b) Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia zitashirikiana na Wizara na Sekta nyingine zinazohusika na Watafiti ili kuangalia Sheria, Taratibu na Kanuni zitakazowezesha kuimarisha shughuli za utafiti Nchini pamoja na kutoa mapendekezo yatakayowezesha matokeo ya utafiti kuwafikia Walengwa.
13. Mheshimiwa Spika, Vilevile, kutokana na majadiliano ya Mkutano huu tulikubaliana kuwa Muundo wa Utafiti na maslahi ya Watafiti yaboreshwe suala ambalo sasa linafanyiwa kazi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta zinazohusika na Watafiti. Aidha, Serikali imeainisha idadi halisi ya Watafiti Nchini ili kuwezesha kuwapanga vizuri katika Muundo Mpya unaoandaliwa. Vilevile, Wadau walikubaliana kukamilisha mapema maandalizi ya Sera ya Maendeleo ya Utafiti.
Maeneo Muhimu ya Kuwekeza Katika Kilimo
14. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo ni kiungo muhimu kwa Sekta nyingine kuchangia zaidi katika ukuaji wa Uchumi wa Taifa letu. Hivyo, hatuwezi kupunguza kiwango cha Umaskini uliopo bila kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Kilimo hapa Nchini hasa kuongeza uzalishaji.Uchambuzi wa Kitaalam unathibitisha kuwa ukuaji wa Uchumi unaotokana na ukuaji wa Kilimo unachangia karibuni mara mbili zaidi katika kupunguza umaskini kuliko unaochangiwa na Sekta nyingine.Ili tuweze kufikia malengo ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo, tunahitaji kuwekeza zaidi ili kuongeza kukua kwa Sekta na kufikia angalau Asilimia 10 kutoka Asilimia 4 ya ukuaji wa hivi sasa.
15. Mheshimiwa Spika, Tunahitaji kuongeza Rasilimali katika Sekta ya Kilimo. Kwa mantiki hiyo na ili kufanikisha utekelezaji wa azma ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini katika kipindi cha mwaka 2010/2011, Serikali inatarajia kuweka kipaumbele katika maeneo yafuatayo:
(a) Kuongeza upatikanaji na Usambazaji wa Pembejeo za Kilimo (Mbolea, Mbegu bora na Madawa);
(b) Kuongeza kasi ya ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji;
(c) Kuimarisha Mashamba ya Uzalishaji Mbegu Bora na Mitamba;
(d) Kuviwezesha Vituo vya Utafiti, kupata Teknolojia sahihi;
(e) Kuimarisha upatikanaji wa madawa ili kudhibiti Visumbufu vya Mimea na Mifugo;
(f) Kuimarisha Mafunzo kwa Maafisa Ugani;
(g) Kuongeza fedha za Mfuko wa Pembejeo za Kilimo;
(h) Kuongeza upatikanaji wa Zana za Kilimo (Matrekta, Plau na Majembe);
(i) Kuimarisha Masoko ya Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi;
(j) Kuimarisha na Kuendeleza Vyama vya Ushirika;
(k) Kuimarisha Miundombinu ya Sekta ya Mifugo Uvuvi;
(l) Kupima na kutenga maeneo ya Kilimo na Ufugaji ili kurahisisha Uwekezaji.
(m) Kujenga na kuimarisha Viwanda vya Kusindika Mazao yatokanayo na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza thamani ya Mazao yetu na hivyo kukuza uchumi wa Taifa letu;
(n) Kuimarisha Miundombinu ya Barabara, Reli na Bandari ili kurahisisha Usafirishaji wa Mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Maeneo haya ni muhimu kama tunataka kupiga hatua katika kuleta Mapinduzi ya Kijani.
MIUNDOMBINU NA USALAMA WA CHAKULA:
16. Mheshimiwa Spika, Usalamawa Chakula Nchini unategemea sana Mtandao mzuri wa Barabara unaopitika kwa urahisi wakati wote kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Barabara Kuu. Hii ni kutokana na ukubwa wa Nchi yetu na kutofautiana kwa uzalishaji wa aina ya Mazao kutoka sehemu moja ya Nchi hadi sehemu nyingine. Vilevile, tofauti ya mtawanyiko wa mvua Kimkoa inayosababisha kutofautiana kwa uzalishaji wa mazao na pia kuwepo kwa maeneo yenye Chakula cha Ziada na maeneo mengine kutokuwa na Chakula. Kwa mantiki hiyo, Mtandao wa Barabara ni muhimu katika kusafirisha Chakula kutoka maeneo yenye Ziada ya Chakula na kupelekwa sehemu yenye Upungufu wa Chakula. Hivyo, Mpango wa kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mazao ya Kilimo Nchini hauna budi kwenda sambamba na uboreshaji wa Mtandao wa Barabara zote Nchini. Maboresho ya Masoko ya Mazao ya Chakula nayo ni muhimu pia.
17. Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli huu, Dira ya Maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2025 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 zimetilia mkazo kwa Serikali kuendelea kuweka kipaumbele cha juu cha Uwekezaji katika Miundombinu, hususan ya Barabara. Serikali za Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne zimeendelea kutambua umuhimu wa Barabara nzuri kama kichocheo cha Ukuaji wa Uchumi na Kupunguza Umaskini, hasa kupitia Sekta ya Kilimo.
18. Mheshimiwa Spika, Katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Miradi 14 ya ujenzi wa Barabara yenye jumla ya Kilometa 1,226 ilianzishwa. Kati ya Miradi hiyo, iliyokamilika katika kipindi hicho ni saba (7) yenye jumla ya urefu wa Kilomita 403. Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani ilirithi Miradi saba (7) yenye urefu wa jumla ya Kilometa 823 ambayo ilikuwa bado kukamilika. Kati ya miradi iliyorithiwa, jumla ya Kilometa 803 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami kufikia mwezi Aprili 2010. Hii ina maana kuwa hadi sasa Miradi yote ya Ujenzi wa Barabara iliyotithiwa kutoka Serikali ya Awamu ya Tatuimekamilika kasoro kipande chenye urefu wa Kilometa 20 kati ya Manyoni na Isuna.
19. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imeanzisha Miradi Mipya 27 ya ujenzi wa Barabara yenye urefu wa Kilometa 1745. Miradi hiyo, sasa inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali.
20. Mheshimiwa Spika, maendeleo haya ya ujenzi wa barabara za lami yamepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo ya usafiri wa Barabara Nchini. Sambamba na hatua hizo za Ujenzi wa Barabara mpya Nchini kwa kiwango cha lami, Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha mtandao wa barabara zote Nchini kwa kufanya matengenezo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuongeza Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Mfuko wa Barabara. Mfuko huo uliimarishwa kwa kuuongezea fedha kwa Asilimia 155 kutoka Shilingi Bilioni 85.74 mwaka 2006/07 hadi Shilingi Bilioni 218.47 mwaka 2007/08 na hali ya Mfuko imeendelea kuwa nzuri hadi sasa.
21. Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza kazi nzuri ambayo imefanyika hadi sasa, katika mwaka 2010/11 hadi 2014/15, Miradi 23 ya ujenzi wa Barabara Kuu kwa kiwango cha lami yenye urefu wa jumla wa Kilometa 2,993 itatekelezwa. Sambamba na Miradi hiyo, ukarabati mkubwa wa Barabara za lami zenye jumla ya Kilometa 853 utafanyika kwa kutumia Fedha za Mkopo wa Benki ya Dunia. Aidha, Fedha za Mfuko wa Barabara zitaongezwa ili kufidia pengo lililopo hivi sasa la mahitaji ya Shilingi Bilioni 435 kwa mwaka kwa ajili ya Matengenezo ya Mtandao wa Barabara Nchini, kutoka kwenye wastani wa Shilingi Bilioni 260 kwa mwaka zinazotolewa hivi sasa.
22. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuunganisha Miji Mikuu ya Mikoa kwa Barabara za lami na Makao Makuu ya Wilaya zote Nchini kwa Barabara za changarawe ifikapo mwaka 2018, kulingana na Mpango Kabambe wa Uwekezaji katika Sekta ya Usafiri na Usafirishaji wa mwaka 2007. Hatua hizo zitachochea sana uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini na hivyo kukuza Uchumi wa Nchi yetu na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.
KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI
23. Mheshimiwa Spika, Uwekezaji katika Kilimo kwa kuhamasisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni sehemu tu ya uhamasishaji tunaofanya katika Uwekezaji kwa ujumla.
Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita Serikali imetekeleza mageuzi makubwa katika Sera za Kusimamia Uchumi Jumla ambazo zililenga katika kujenga Uchumi wa Soko na kuifanya Sekta Binafsi kuwa Injini ya ukuaji wa Uchumi. Kutokana na mageuzi hayo, Serikali ilijitoa katika shughuli za moja kwa moja za kufanya Biashara na kujielekeza zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya Dola, ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya Sera na Sheria ikiwa ni pamoja na Miundombinu ya msingi kwa ajili ya kuvutia Wawekezaji na ukuaji wa Sekta binafsi iliyo imara na endelevu.
24. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali imetekeleza Programu mbalimbali za kuleta mageuzi katika Sekta ya Umma, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Usimamizi wa Fedha na Bajeti ya Serikali, Sheria, Utawala Bora pamoja na Sekta za Kitaaluma za Elimu, Afya, Maji na Ardhi. Programu zote hizi zimelenga Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini, pamoja na kuboresha mazingira ya kufanya biashara Nchini na kuvutia Wawekezaji.
25. Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Programu hizo, kumekuwepo na mafanikio ya kuridhisha katika Ukuaji wa Uchumi na Uwekezaji. Kwa mfano, tangu mwaka 2000 hadi 2008 Uchumi wetu umekua kwa kiwango cha Wastani wa Asilimia 5 mpaka 7 kwa mwaka. Aidha, Uwekezaji wa Mitaji ya Moja kwa moja umeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 150.86 Milioni mwaka 1995 hadi Dola za Kimarekani Milioni 695.5 mwaka 2008. Pamoja na mafanikio hayo, bado kasi na kiwango cha ukuaji wa Uchumi wetu pamoja na Uwekezaji hakikidhi mahitaji na malengo ya kuondoa Umaskini. Kasi ya Ukuaji wa Uchumi na Uwekezaji inahitajika kuongezeka zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho Uchumi wa Dunia umepata msukosuko wa Kifedha na hivyo kuongeza ushindani wa kuvutia Wawekezaji.
26. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa tuliyopata awali katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tangu mwaka 2007 kumekuwepo na mwenendo usioridhisha wa Mazingira ya Uwekezaji na Biashara Nchini. Katika tathmini iliyofanywa na Benki ya Dunia mwaka 2009 kuhusu Hali ya Wepesi wa kufanya Biashara katika Nchi mbalimbali Duniani, Taarifa inaonyesha kuwa katika Viashiria 10 vilivyotumika, Tanzania imeshika nafasi ya 131 miongoni wa Nchi 183 zilizofanyiwa Tathmini. Nafasi ya Tanzania mwaka huu ni ya chini ikilinganishwa na Nchi jirani katika Ukanda wetu ambazo zimewekwa katika nafasi zifuatazo: Rwanda (67); Kenya (75); Zambia (90) na Uganda (112). Aidha, taarifa za miaka ya nyuma zinaonyesha kuwa Tanzania ilishika nafasi ya 124 mwaka 2007 na nafasi ya 127 Mwaka 2008. Nchi ya kwanza Duniani kwa Wepesi wa kufanya Biashara na Uwekezaji ni Singapore.
27. Mheshimiwa Spika, Mchanganuo waViashiria kumi (10) vilivyotumika kuandaa taarifa ya jumla ya wepesi wa kufanya Biashara na nafasi ya Tanzania kwa kila kiashiria kuhusu hali ya ufanisi wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji ikilinganishwa na Nchi nyingine ni kama ifuatavyo:
|
Viashiria
|
Nafasi ya Tanzania
|
|
i) Uanzishaji wa Biashara
|
120
|
|
ii) Vibali vya Ujenzi
|
178
|
|
iii) Ajira ya Wafanyakazi
|
131
|
|
iv) Usajili wa Rasilimali zisizohamishika
|
145
|
|
v) Upatikanaji Mikopo
|
87
|
|
vi) Ulinzi wa Wawekezaji
|
93
|
|
vii) Ulipaji Kodi
|
119
|
|
viii) Wepesi wa Biashara ya Nje
|
108
|
|
ix) Kulinda Mikataba
|
31
|
|
x) Usitishaji au Kufunga Biashara
|
113
|
|
xi) Wastani wa Urahisi wa Kufanya Biashara
|
131
|
28. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kufikirika kuwa inachukua siku 328 kupitia taratibu 22 tofauti kupata kibali cha kujenga Ghala dogo.
29. Mheshimiwa Spika, Serikali imetafakari kuhusu mwelekeo wa kuendelea kushuka kwa Tanzania katika Viashiria vya Kimataifa vya Wepesi wa Mazingira ya Uwekezaji kufanya Biashara Nchini na kuona kuwa hauendani na juhudi kubwa za Serikali za utekelezaji wa Mageuzi makubwa ya Kiuchumi na Kijamii yanayoendelea kufanyika kupitia Maboresho mbalimbali ya Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu; pamoja na utekelezaji wa Programu mbalimbali za Kisekta chini ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini. Vilevile, mwenendo huo hauendani na dhamira ya Serikali ya kuifanya Sekta Binafsi kuwa Injini ya Ukuaji wa Uchumi na kuleta Maendeleo endelevu Nchini. Kwa maana hiyo, tangu Mwezi Septemba 2009 Serikali imeunda Kikundi Kazi cha Makatibu Wakuu ambacho kimesimamia Uchambuzi wa vikwazo vilivyopo kwa lengo la kuchukua hatua za haraka.
30. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa hadi sasa Kikundi Kazi cha Makatibu Wakuu kimekamilisha kazi yake na kuandaa Taarifa ambayo imewasilishwa Serikalini kwa hatua zaidi. Aidha, tayari Serikali imeanza kutekeleza baadhi ya hatua zilizopendekezwa ikiwa ni pamoja na Taratibu za Taarifa ya thamani za mali (Property Valuation Report) na kaguzi zinazofanywa na Wataalam mbalimbali. Lengo la Serikali ni kufanya mapitio ya kina ya Sheria na Kanuni zinazochangia kuwepo kwa Vikwazo vya Uwekezaji na biashara hasa katika maeneo ya upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi, kuanzisha Biashara, kupata Mikopo, Ulipaji wa Kodi, kuajiri Wafanyakazi, Uandikishaji wa Rasilimali, kulinda Mikataba na Wepesi wa Biashara ya Nje hasa kurahisisha mchakato wa kupitisha na kugomboa mizigo Bandarini na katika Vituo vya Forodha. Ninayasema haya ili Watanzania wote tuweze kuona uzito wa suala hili na kwa pamoja tuweze kubadilika na kurejesha hadhi ya Nchi yetu.
31. Mheshimiwa Spika, pamoja na marekebisho ya Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu ambayo yanahitajika kufanyika katika Sekta zote, napenda kusisitiza kuwa, ili Tanzania iweze kupiga hatua katika kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini, ni muhimu tujizatiti kikamilifu kukabiliana na Changamoto zifuatazo:
Help | Disclaimer | Privacy | Site Feedback
Copyrights ©2008-2010, The United Republic of Tanzania, Prime Minister All Rights Reserved
Designed and published by DataVision International (T) Ltd |