HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ALIYOITOA KATIKA SHUGHULI YA KULIPONGEZA BUNGE NA SERIKALI KWA KUPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA MTOTO 2009 TAREHE 17 APRILI, 2010 JAMHURI STADIUM, DODOMA
Mheshimiwa Margareth Sitta, (Mb.), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto;
Mheshimiwa Dkt. James Msekela, (Mb.), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge;
Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Mkurugenzi wa Asasi ya Kusaidia Vijana na Watoto - Dodoma
Ndugu Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama na Dini;
Ndugu Viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali;
Watoto Wapendwa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Utangulizi
Kwanza kabisa, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye tukio hili la Kulipongeza Bunge letu Tukufu na Serikali kwa kupitisha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009. Sheria ambayo ilipitishwa na Bunge katika Mkutano wa 17 mwezi Novemba 2009 na baadaye kusainiwa na Mheshimiwa Rais na hivyo kuanza kufanya kazi rasmi tarehe 01 Aprili, 2010.
Pili, nazishukuru sana Asasi zote zilizopo Mkoani Dodoma kwa ushirikiano mkubwa mliouonyesha hadi kufanikisha kuandaa shughuli hii ambayo inawawakilisha Watoto wote wa Tanzania. Ushirikiano huu ni mfano mzuri wa kuigwa na Asasi nyingine Nchini katika kutekeleza jambo lolote lenye maslahi kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla. Niwapongeze kwa namna ya kipekee Asasi ya Kusaidia Vijana na Watoto - Dodoma (Dodoma Youth and Children Support Foundation) walioanzisha wazo hili na kushirikisha Baraza la Watoto. Nawashukuru Wadau wengine kwa kulipokea na kuliboresha mpaka kufikia hatua hii ya kuwa na Shughuli hii leo. Tunaushukuru pia Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuratibu shughuli hii. Tunawashukuru sana Watoto waliojitokeza leo hii, Walimu wao na Wananchi kwa ujumla. Hakika mmeifanya siku ya leo iwe ya kupendeza na imefana sana!
Umuhimu wa Sheria ya Watoto
Ndugu Wananchi,
Hapo awali hatukuwa na Sheria moja mahususi kwa ajili ya Watoto bali tulikuwa na Sheria Tano (5) ambazo zilifutwa na zingine Tano (5) ambazo zilifanyiwa marekebisho. Sheria zote hizi ziligusa haki na ustawi wa Watoto kwa namna moja ama nyingine. Hali hii ilisababisha matatizo mengi kwa Wadau katika kusaidia Watoto. Kwa hali hiyo, na kwa tukio la leo, inastahili kuipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kuratibu jitihada zilizofanyika mpaka kuhakikisha kuwa kunakuwepo Sheria hii ya Mtoto ya Mwaka 2009. Inategemewa kuwa utekelezaji wa Sheria hii utazingatia zaidi upatikanaji wa Haki za Msingi za Watoto na kuendeleza ustawi wao. Nitumie fursa hii kuzipongeza Wizara zingine zilizoshiriki katika maandalizi ya Sheria hii zikiwemo Asasi Zisizo za Kiserikali (NGOs). Kwa njia ya pekee tunaishukuru sana UNICEF kwa ushirikiano wake wa karibu.
Ndugu Wananchi,
Uko ukweli kwamba, baadhi ya Watoto wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi zikiwemo Haki ya Kuishi, Haki ya Kuendelezwa, Haki ya Kulindwa na Kutunzwa. Vilevile, baadhi ya Watoto walikuwa wakikosa Haki ya Kushiriki katika masuala yanayowahusu na Haki ya kutobaguliwa.
Tumesikia mara kadhaa baadhi ya Watoto wakinyimwa haki hizo kwa kukatishwa uhai wao, kunyanyaswa, kudhulumiwa na kunyimwa haki zao za kimsingi. Aidha, baadhi ya Watoto wamekuwa wakitendewa maovu bila huruma kama vile, kubakwa na kulawitiwa. Baadhi ya Watoto wamekuwa wakikatishwa masomo kwa kuozwa katika umri mdogo, kupigwa, kutumikishwa kazi ngumu, kuchunga Mifugo badala ya kusoma na kutelekezwa bila msaada wowote. Mara nyingine vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na Wazazi au Walezi na baadhi ya Wanafamilia wa Watoto hao bila huruma na wala aibu.
Kwa Watoto wetu, napenda kuwahakikishia kwamba kilio chenu kimesikika. Sheria hii ni ukombozi wenu. Sheria hii inataja bayana Haki zenu za Msingi ambazo ni:
i) Haki ya kutokubaguliwa;
ii) Haki ya kuwa na Jina, Utaifa, na kuwatambua Wazazi na Ndugu wa Ukoo;
iii) Haki ya kuishi na Wazazi wenu au Walezi pale ambapo Wazazi hawapo;
iv) Haki ya Kurithi Mali ya Wazazi;
v) Haki ya kutoa mawazo na kusikilizwa kulingana na Umri; na
vi) Haki ya Elimu na kuendelezwa.
Serikali itahakikisha kwamba Sheria hii inatekelezwa ili kudhibiti maovu mengi mnayotendewa. Napenda kutoa tahadhari kwamba kuanzia sasa tunapoanza utekelezaji wa Sheria hii kwamba, yeyote atakayebainika kuendeleza vitendo viovu kwa Watoto atakuwa amegusa Mboni ya Jicho la Serikali. Adhabu kali itatolewa kwa yeyote atakayehusika na ukatili wa aina yoyote dhidi ya Watoto. Kwa wale waliojenga mazoea ya kuwaonea Watoto sasa waache mara moja, kwa sababu Sheria hii sasa itachukua Mkondo wake.
Nawaomba Wananchi wote kwa ujumla kuipitia na kuielewa Sheria hii vizuri. Matarajio ni kwamba, Sheria hii itatafsiriwa katika lugha ya Kiswahili ili Wazazi, Walezi na jamii nzima waweze kuisoma kwa urahisi na hivyo wajue wajibu wao kwa Watoto. Aidha, adhabu kali zitatolewa dhidi ya wale ambao watashindwa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria hii.
Jukumu la Wazazi
Ndugu Wananchi,
Matunzo na malezi ya Watoto ni muhimu sana kwa Taifa kwani maadili mema ya Taifa yatatokana na matunzo na malezi ya Watoto leo. Wote tumesikia Msemo wa Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo”. Hii ni kwa ajili ya Malezi ya Tabia. Lakini pia tunajua kwamba, Mbegu ambayo tunaipanda leo ndiyo tutakayoivuna kesho. Kwa mantiki hiyo, kutimiza wajibu wetu wa Malezi Bora kwa Watoto leo ni kutafuta Amani, Upendo na Maisha Bora kwa Watoto wetu kwa siku zijazo.
Ndugu Wananchi,
Kama Wazazi na Walezi, tunao wajibu wa kulea Watoto wetu ipasavyo. Tunao wajibu wa kuwapatia mahitaji yao muhimu. Tunao wajibu wa kuwawekea mazingira mazuri ili waweze kufikia mafanikio yanayotarajiwa. Kwa mfano, wako Watoto walioko kwenye Shule za Msingi na wengine Shule za Sekondari. Ni wajibu wa kila Mzazi na Mlezi kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji muhimu ikiwemo Chakula cha Mchana kwa Wanafunzi wa kutwa. Ni wajibu wa Wazazi na Walezi kuchangia Chakula cha Mchana ili Watoto hawa waweze kuzingatia Masomo kadri inavyotakiwa. Napenda kutumia nafasi hii kusisitiza umuhimu wa kuwapatia Watoto Chakula cha Mchana au Kipooza Njaa. Kwa kufanya hivyo tutaboresha matokeo yao, na hivyo kupata Wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika Mitihani wanayofanya.
Napenda kusisitiza kwamba, suala la kuwapenda Watoto wote bila kuwabagua kijinsia, dini au kabila sasa ni suala la Kisheria. Tuwape haki zao zote za msingi zikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa kielimu na mafunzo. Tuwape haki zao za kutunzwa, kufundishwa maadili mema, kutobaguliwa na kushirikishwa katika mambo yanayowahusu kulingana na umri wao. Wazazi, Walezi na Wananchi wote tuwajibike katika kuwalea Watoto wetu ili kuwatengenezea Maisha Bora ya baadaye.
Jukumu la Mtoto
Kwa Watoto wetu,
Tumekusanyika hapa kulipongeza Bunge na Serikali kwa kupitisha Sheria ya Mtoto. Katika Sheria hii, nanyi Watoto mna wajibu wa kutekeleza. Kama Watoto mnawajibika kulinda na kuendeleza mila, desturi na maadili mema kama vile mnavyoelekezwa na Wazazi, Walezi na kutoka kwa Walimu wenu. Mnatakiwa kupenda kujiendeleza kielimu, kuepuka Matumizi ya Dawa za Kulevya, kutofanya biashara ya ukahaba na kuacha kuzurura ovyo au kuishi mitaani. Vilevile, mna wajibu wa kuwatii, kuwaheshimu na kuwapenda Wazazi na Walezi wenu na jamii kwa ujumla. Ni wajibu wenu kuonyesha kwa vitendo maadili mema yanayozingatia yale mnayofunzwa na Wazazi na Walezi wenu. Mlioko Shuleni, ni wajibu wenu kufuata maelekezo ya Walimu wenu. Aidha, kwa kupitia Mabaraza na Vikundi vya Watoto mnao wajibu wa kushiriki na kuchangia kwa mawazo na vitendo katika mipango na mikakati ya Taifa ili kuboresha maendeleo yenu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Ninyi ndiyo Viongozi watarajiwa wa Taifa letu. Kwa maana hiyo, ni lazima kuzingatia malezi na maadili mema yatakayowawezesha kuongoza kizazi kijacho. Wekeni bidii kwa kila jambo zuri mnalofundishwa. Onyesheni uwezo wenu na Vipaji vyenu ili Wazazi na Walezi wenu, Walimu na Jamii kwa ujumla iweze kuwabaini. Kwa njia hiyo mtaweza kujitengenezea Maisha Bora ya baadaye.
Jitihada za Serikali katika kulea Watoto.
Ndugu Wananchi,
Leo tumeshuhudia pongezi zenu ninyi Watoto kwa Bunge na Serikali kuhusu kupitishwa kwa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009. Kupitishwa kwa Sheria hii, ni moja tu ya jitihada za Serikali katika kuboresha Maisha ya Mtoto. Jitihada ziko nyingi. Kwa mfano, tayari Serikali inayo Sera ya Afya inayohusu Matibabu bure ya Watoto wote wenye umri wa miaka 0-5 ambayo tayari inatekelezwa. Vilevile, ipo Mipango ya Kitaifa ya Huduma ya Afya kwa Mtoto ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo mbalimbali bure na hata huduma za Afya Shuleni.
Kwa upande wa Elimu Serikali imeweka Sera ya kila Mtoto lazima apate Elimu ya Msingi. Hii ni haki ya lazima kwa kila Mtoto. Kwa maana hiyo, Serikali imejenga Shule za Msingi na Sekondari na kuhakikisha kwamba kila Mtoto aliye na umri wa kwenda Shule anapata nafasi ya kusoma na kila atakayefaulu katika mtihani wa Darasa la Saba anapata nafasi ya kujiunga na Kidato cha Kwanza. Aidha, Serikali imeweka Sera ya Ada Ndogo kwa Sekondari ili Watoto wengi zaidi wapate nafasi ya kupata Elimu ya Sekondari. Hizi zote ni juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watoto wote wanapata Haki za Msingi katika kujenga maisha yao. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba Sera na Mikakati tunayojiwekea kuhusu Maendeleo ya Mtoto zinatekelezwa.
Kushirikiana Katika Malezi
Ndugu Wananchi,
Kuna umuhimu wa kushirikiana katika Malezi ya Watoto wetu kati ya Serikali na Mashirika mbalimbali, Asasi Zisizo za Kiserikali, Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla. Kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na Mashirika mengi Yasiyokuwa ya Kiserikali ikiwemo kazi hii ya leo, ninatoa wito kwa Watendaji wa Serikali wa ngazi zote, kutoa ushirikiano kwa Mashirika haya ili kuwatia moyo katika majukumu yao waliyojipangia. Majukumu ambayo wakisaidiwa kutekeleza vizuri, Watakuwa wamechangia katika nguvu za Serikali za kuweka Maisha Bora kwa Watoto wetu. Suala la kuwatunza Watoto ni letu sisi sote.
Serikali peke yake haiwezi. Tusaidiane katika kuwafichua wanaowanyima Watoto wetu haki zao, kwani sasa tunayo Sheria inayowalinda Watoto. Wote tushirikiane na Asasi Zisizo za Kiserikali na jamii yote kuendelea kusaidiana na Serikali kuhakikisha kuwa Watoto wanapata haki zao kwa kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili dhidi yao. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewapa Watoto haki zao stahili na kuendeleza ustawi wao kwa maisha yao.
Mwisho
Ndugu Wananchi,
Nimalizie kwa kuwashukuru tena wote walioshiriki katika kuifanikisha shughuli ya leo. Nimevutiwa sana na paredi ya Watoto, Nyimbo nzuri zenye kutoa taswira nzuri ya Uzalendo kwa Nchi yetu. Nimevutiwa pia na Ngonjera na Maigizo yenye mafundisho na maonyo kwa Wazazi na Walezi wasiowajali Watoto. Nawapongeza sana kwa Maandalizi mazuri ya kihistoria.
Mwisho, natoa wito kwa Wazazi, Walezi na Mashirika yote, Taasisi za Dini na Wananchi kwa ujumla kuendelea kuwapa Watoto mahitaji yao yakiwemo haki zao za msingi. Serikali na Bunge tutaendelea kushirikiana ili kubuni njia mbalimbali za kuhakikisha kuwa Watoto wa Tanzania wanaendelea kupata haki zao kwa manufaa yao na Taifa kwa jumla. Kwa Kupenda Watoto, Tutimize Wajibu Wetu!
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA. |