HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), WAZIRI MKUU, KATIKA HAFLA YA KUFUNGA KONGAMANO LA UTUMISHI WA UMMA TAREHE 18 JUNI 2008
Mheshimiwa Hawa A. Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma;
Bwana Eric Mothibi Molale, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu wa Baraza la Mawaziri na
Mkuu wa Utumishi wa Umma wa Serikali ya Jamhuri ya Botswana;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Wawakilishi wa Nchi Mbalimbali;
Wahisani wa Maendeleo;
Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waandaaji wa Kongamano hili la Kitaifa kuhusu Maboresho ya Sekta ya Umma kwa kunialika kuwa Mgeni katika hafla ya kufunga Kongamano hili.
Pia nimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemon L. Luhanjo, ambaye ndiye aliyeitisha Kongamano hili. Niwashukuru pia Watumishi wote Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakiongozwa na Mheshimiwa Hawa A. Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi, pamoja na Bwana George Yambesi, Katibu Mkuu, kwa kuandaa na kufanikisha Kongamano hili.
Nitumie nafasi hii pia kuwashukuru wote kwa kuhudhuria na kushiriki kwenye Kongamano hili muhimu la Kitaifa. Nimejulishwa kwamba Kongamano hili limejuimuisha Washiriki kutoka Sekta mbalimbali ambao ndio Wadau wa Sekta ya Umma. Wapo Wanataaluma, Wawakilishi wa Sekta Binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Viongozi na Watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali wanaowakilisha Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mikoa, Wilaya na Serikali za Mitaa.
Uwakilishi huu mpana unaashiria kwamba Washiriki mmepata nafasi ya kujadili kwa kina mada mbalimbali zilizowasilishwa kwenye Kongamano hili. Ni matarajio yangu kwamba Maazimio na Mapendekezo yaliyotolewa kwenye Kongamano hili yatafanyiwa kazi ili kuweza kuboresha zaidi Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yake ya kuhudumia Wananchi. Vilevile, kwa kufanya hivyo kutawezesha Utumishi wa Umma kuchangia ipasavyo katika ukuzaji wa uchumi wa Nchi yetu na kupunguza umaskini kama ilivyo ainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Nitambue kuwepo kwa Bwana Eric Mothibi Molale, Katibu Mkuu wa Rais na Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma wa Serikali ya Jamhuri ya Botswana, ambaye nimejulishwa kwamba tulimwalika rasmi kutoa Mada kuu kuhusu uzoefu wa Nchi ya Botswana na mafanikio waliyoyapata katika kutekeleza Maboresho ya Sekta ya Umma. Ninapenda kumshukuru na kumpongeza kwa kuitikia mwaliko wa kuja Tanzania na kubadilishana nasi uzoefu wao wa namna wanavyoyakabili na walivyofanikiwa na pia changamoto ambazo bado zinawakabili katika kutekeleza Maboresho mbalimbali katika Sekta ya Umma. Nina hakika Watanzania tulioshiriki katika Mada yake tumejifunza mengi ambayo tunaweza kuyatumia katika mazingira ya Nchi yetu ili tuweze kutekeleza na kufanikisha Maboresho ya Sekta ya Umma vizuri zaidi, na kupata matokeo tunayotarajia. Honourable Molale, thank you very much for coming to share with us the experiences from your country. Asante Sana!
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Ninaelewa na kutambua kwamba Kongamano limejadili kwa kina maeneo mengi muhimu na kupata michango kutoka kwa Washiriki wenye upeo na uzoefu kuhusu Utumishi wa Umma. Hata hivyo, bila kutaka kuharibu matokeo ya majadiliano yenu mliyoyafanya jana na leo, nami ningependa nitumie fursa hii mliyonipatia kuja kufunga Kongamano hili ili niweze kuzungumza mtazamo nilionao kuhusu Maboresho ya Sekta ya Umma na nitafanya hivyo kwa ufupi tu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Kwa kuangalia maudhui ya Kongamano hili ambayo nakala yake nimeisoma, madhumuni ya msingi ya Kongamano yalikuwa ni kuainisha, kujadili na kuchambua sababu zinazofanya utekelezaji wa Maboresho katika Sekta ya Umma hapa Nchini usiwe wa kuridhisha kwa maana ya kasi ya utekelezaji wa matokeo. Sina shaka kwamba baadhi ya sababu zilizoainishwa ni pamoja na matatizo na changamoto za Uongozi mahiri, Maadili na ukosefu wa uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.
Sababu hizi, kila mojawapo au kwa pamoja ndizo kwa kiwango kikubwa zimeathiri utekelezaji wa Maboresho ya Sekta ya Umma hapa Nchini. Kwa maneno mengine, Maboresho ya Sekta ya Umma ambayo tunayatekeleza kwa karibu miaka ishirini sasa, hayajaleta mafanikio yaliyokusudiwa kwa sababu ya kutokuwepo kwa Uongozi Mahiri katika ngazi mbalimbali za Utumishi wa Umma kwa upande mmoja na ukosefu wa Maadili, Uadilifu na Kutowajibika kwa upande mwingine.
Kwa hakika, majawabu ya matatizo haya sio mepesi. Hata hivyo, naamini kabisa kuwa endapo hatua za makusudi zitachukuliwa kwa kuandaa Mikakati endelevu ya Viongozi watakaoshika madaraka katika ngazi mbalimbali; kuimarisha mifumo ya uwajibikaji katika ngazi ya Mtumishi binafsi na kwa Taasisi pamoja kuhakikisha uzingatiaji wa Maadili na Uadilifu katika Utumishi wa Umma, mafanikio yanaweza kupatikana tena kwa haraka zaidi.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Katika kuchangia nisingependa kurudia tena mada mlizokwisha kuzijadili kwa kina mapema. Hata hivyo, niongee kwa kifupi uzoefu wa Nchi nyingi za Kiafrika kwa maeneo ambayo yanaweza kusababisha kupata au kushindwa kupata mafanikio katika Maboresho ya Sekta ya Umma:
Kwanza, ili Maboresho yaweze kufanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa, ni lazima kuwepo na umiliki na dhamira ya pamoja ya kutekeleza Maboresho kutoka kwa Viongozi wa ngazi za juu wa Kisiasa wa Kitaifa na Viongozi Watendaji katika Taasisi za Umma hadi kwa Watumishi wa Umma. Viongozi ndio wanaoweza kusababisha kuwepo au kutokuwepo kwa mafanikio katika kuboresha utendaji katika Utumishi wa Umma. Ili kupata ushirikiano wa Viongozi wa Kisiasa wa ngazi mbalimbali, ni vyema Taasisi zinazohusika na Maboresho zitoe fursa za kuwaelimisha na kuwashirikisha Wanasiasa ili waweze kuelewa vizuri mahusiano yaliyopo kati ya Maboresho na utoaji wa huduma kwa Wananchi kwa kuzingatia Agenda kuu za Kitaifa kama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005.
Pili, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Halmashauri za Serikali za Mitaa ndio wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa Maboresho ya Sekta ya Umma. Ili kuwezesha umiliki, ni lazima utekelezaji wa Maboresho uwe ni sehemu ya kazi zetu za kawaida katika Taasisi zetu. Ili kuimarisha uwajibikaji, utendaji wenye tija na ufanisi katika matumizi ya raslimali za umma, Taasisi za Umma zinapaswa kuhakikisha utekelezaji wa Maboresho unakuwa ni sehemu ya Mipango yetu ya utekelezaji na Mipango Mikakati ya kila mwaka.
Tatu, ninahakika mtakuwa mmejadili kuhusu utekelezaji wa Programu za Maboresho na kwamba lazima usaidie kubadilisha namna tunavyotoa huduma. Ieleweke kwamba matarajio ya Wananchi kuhusu Maboresho tunayoyatekeleza ni kupata huduma bora zaidi, kwa uharaka na bila urasimu. Kwa hiyo basi, ni muhimu pia matokeo ya utekelezaji wa Maboresho uwezeshe Utumishi wa Umma kuhudumia Wananchi kwa ‘Ari, Nguvu na Kasi Mpya’.
Kwa upande mwingine, ili kujenga Utumishi wa Umma wenye usikivu zaidi, hatuna budi kushirikiana hata na Taasisi Zisizo za Kiserikali pamoja na Sekta Binafsi kuzishirikisha na kuzielimisha Taasisi hizo kuhusu Maboresho. Lengo ni kuzisaidia ili nazo ziweze kutoa msukumo zaidi kwa Taasisi za Umma kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuhudumia Wananchi vizuri zaidi na kwa usikivu na staha.
Nne, uwajibikaji mzuri unategemea sana uelewa wa yale yanayotekelezwa na Serikali kwa Wadau wake. Ili kujenga uwajibikaji, kunahitajika sana kuwepo kwa Daraja la Mawasiliano kati ya Taasisi mbalimbali za Serikali na Wananchi. Nazipongeza Taasisi mbalimbali za Serikali na zile za Binafsi kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuelimisha Umma kuhusu haki zao na wajibu wa Serikali katika kujenga Mawasialino ya dhati. Pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto ya kujenga uelewa thabiti wa kazi za Serikali, namna ya kupata huduma, namna ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, namna ya kulalamika pale ambapo mambo hayaendi vizuri na kushinikiza mabadiliko ya kweli na huduma bora pale ambapo kunaonekana kuwepo na ubabaishaji.
Tano, Suala la Elimu kwa Umma linahitaji Mkakati mzuri wa mawasialino kati ya Serikali na Wadau wake. Kwa kuwepo na mkakati kama huo, Utumishi wa Umma utakuwa na usikivu zaidi, uwazi na kuwajibika kwa Wananchi na hivyo kuimarisha dhana nzima ya Utawala Bora. Katika kukamilisha hili, ni vizuri Wadau mbalimbali, hasa wale wanaofanya kazi kwa karibu na Wananchi kama Vyombo vya Habari, Taasisi Zisizo za Serikali na Mashirika ya Kidini kushirikishwa kikamilifu katika jitihada hizi. Pia matumizi ya kimkakati ya uwajibikaji ya nyenzo kama Mikataba ya Huduma kwa Mteja yasisitizwe na utumiaji wake ujengewe uelewa wa hali ya juu kwa Wadau. Vilevile, Ufuatiliaji na Tathmini ya matumizi yake ufanyike mara kwa mara na matokeo yake yatumike kuboresha huduma kwa Wananchi. Napenda kusisitiza kwamba Suala la Elimu kwa Umma ni muhimu kwa Wananchi tunaowaongoza. Ni wajibu wa Watumishi wa Umma kuwajulisha Wananchi haki mbalimbali za kuhudumiwa na Watumishi wa Umma. Ni lazima tuendelee kuwafahamisha juu ya Wajibu wa Utumishi wa Umma kwao katika kutoa huduma, kusimamia fedha, maadili ya Utumishi wa Umma, n.k. Wasipojua hayo yote, watashindwa kuwezesha Watumishi kupimwa ipasavyo.
Sita, juhudi za kuboresha Sekta ya Umma zinapaswa kujikita zaidi katika maeneo ambayo matokeo yake yatasaidia na kuchangia kwa haraka katika kuboresha huduma kwa Wananchi pamoja na kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Maboresho yanayolenga kuboresha mifumo mbalimbali ya utendaji na Maboresho ya Kisekta kama Afya, Elimu, Maji na mengineyo, yanapaswa kutekelezwa katika namna ambayo itakuwa inajibu matakwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, MKUKUTA pamoja na malengo yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005.
Saba, ni dhahiri kwamba bila ya kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa yale tuliyopanga ili kufahamu utekelezaji wa malengo yetu itakuwa tunapoteza raslimali na kodi za Wananchi bure. Upo msemo unaosema ”If you can’t measure it you can’t Manage it”.Tafsiri yake ni kwamba, bila kupima utekelezaji wa malengo yaliyowekwa itakuwa ni vigumu kufahamu kama unafanikiwa au la. Kufuatilia na kutathmini utendaji na utekelezaji, kunachangia sana katika kuimarisha dhana ya uwajibikaji katika ngazi ya Mtumishi binafsi na Taasisi kwa ujumla.
Ninapenda kutumia fursa hii kusisitiza kwamba Taasisi za Umma zote zihakikishe kwamba zinakuwa na mfumo wa kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa malengo yao wakati wote. Kwa kuwa dhana hii inahusiana na uboreshaji wa mifumo ya utendaji kazi, matumizi ya raslimali pamoja na utoaji wa Taarifa za Utekelezaji, ninaziagiza Wizara ya Fedha na Uchumi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuimarisha matumizi ya mfumo wa Tathmini na Ufuatiliaji. Kuimarika kwa mfumo wa kutathmini na ufuatiliaji kutaimarisha utekelezaji wa Sera na Mipango mbali mbali ya Serikali, pamoja na uwajibikaji kwa Watendaji katika Taasisi za Umma.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Hayo ndiyo maeneo machache niliyopenda kuyazungumzia kwa ufupi. Inawezekana nimerudia baadhi ya yale mliyokwishajadili, lakini, endapo mtakuwa mliyajadili basi kurudia kwangu mchukulie kama ni kuendelea kuyawekea msisitizo zaidi!
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Nirudie kuwashukuru kwa kushiriki Kongamano hili. Nawatakia kheri mnaporejea katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku. Baada ya kusema hivyo, sasa napenda nichukue nafasi hii kutamka kwamba Kongamano la Kitaifa kuhusu Maboresho ya Sekta ya Umma limefungwa rasmi.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA! |