Home >Speech
Speech
mgPrint friendly version mg Email this page

Hotuba ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, (Mb.), Kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu Na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2008/2009

UTANGULIZI

1.  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliyochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2007/2008 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2008/2009. Aidha, naliomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zilizo chini yake na yale ya Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2008/2009.

 

2.  Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyonipa kuniteua kuwa Msaidizi wake wa karibu wa kuongoza shughuli za Serikali ya Awamu ya Nne. Nawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge chini ya uongozi wako kwa kuthibitisha uteuzi wangu kwa kura nyingi.

 

Changamoto zilizo mbele yetu ni nyingi, lakini imani yenu kubwa kwangu na ushirikiano mnaoendelea kunipa, unanipa moyo kwamba kwa pamoja tutaweza kukuza uchumi, kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za jamii na hatimaye kuleta maisha bora kwa Watanzania.

 

3. Mheshimiwa Spika, mwezi Mei 2008, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri. Katika mabadiliko hayo, Mheshimiwa Rais alimteua Mheshimiwa Celina Kombani (Mb.), kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Profesa Peter Msolla (Mb.), Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia; Mheshimiwa Dk. Shukuru Kawambwa (Mb.), Waziri wa Miundombinu na Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.), kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Aidha, alimteua Mheshimiwa Aggrey Mwanri (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa, Hezekiah Chibulunje (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu na Mheshimiwa Dk. Milton Makongoro Mahanga (Mb.), kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana. Napenda kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kuteuliwa kwao kushika nyadhifa hizo muhimu.

 

4. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Bunge lako tukufu lilipata msiba wa marehemu Salome Mbatia aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na marehemu Benedict Losurutia aliyekuwa Mbunge wa Kiteto. Nichukue fursa hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa familia za marehemu hao. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

 

5. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kisichopungua siku tano Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakijadili taarifa kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 na Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2008/2009 na hatimaye kuipitisha. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo, (Mb.), Waziri wa Fedha na Uchumi kwa hotuba yake nzuri na jinsi alivyoweza kutoa maelezo ya ufasaha kuhusu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri na michango yenu mizuri mliyoitoa wakati wa majadiliano ya Bajeti ya Serikali. Ninawahakikishia kwamba michango hiyo itazingatiwa wakati wa utekelezaji.

 

6.Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa kupitia Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge. Ninazishukuru sana Kamati za Kudumu za Bunge lako tukufu kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Matumizi ya kila Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na taasisi zilizo chini ya wizara zote.

 

7. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali mliyoipitisha ndiyo itakayotuwezesha kuendesha kazi za Serikali na kutekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005. Bajeti hiyo imezingatia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo 2025, Malengo ya Milenia 2015 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA). Serikali itaendelea kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato kwa kutekeleza miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi za Serikali zinazojitegemea zimetengewa fedha kulingana na majukumu waliyo nayo ambayo yanalenga kutekeleza MKUKUTA. Viongozi na watendaji wote wa Serikali wanao wajibu wa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kazi zilizopangwa na kutoa taarifa za utekelezaji kwa mamlaka husika. Ufuatiliaji huo, ukishirikisha  wananchi, utaongeza uadilifu na uwajibikaji wa watendaji katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo. Natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha wananchi kuhusu bajeti hii na miradi itakayotekelezwa katika maeneo yao.

 

Mwandishi mmoja Glenn Bland aliandika: “Goals and plans take the worry out of living.” Kama tukiweka malengo, hatua tunazozichukua zitazingatia maisha tunayoyahitaji badala ya kutegemea kila tunapoamka asubuhi tunajisikiaje. Tumepanga, tumekadiria na tunategemea kutumia. Mipango yetu itafanikiwa kama tutatumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya kile kilichopangwa.

 

HALI YA SIASA

 

8.   Mheshimiwa Spika, nchi nyingi duniani zimekuwa na mafanikio ya uchumi imara kutokana na kujiwekea misingi  bora ya hali ya siasa, amani na utulivu. Aidha, uchumi imara ni matokeo ya juhudi wanazowekeza wananchi katika uzalishaji mali kwenye nchi inayozingatia utawala wa sheria na yenye sera nzuri za uwekezaji. Ninayo furaha kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba, nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimepata sifa kubwa katika kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za kiitikadi zilizopo. Napenda kuwapongeza wananchi wote kwa kushiriki katika kudumisha amani na utulivu nchini. Nawahimiza kuzidi kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika bara letu la Afrika na duniani kote. Nawasihi tusiichezee sifa hii, kwani tukiipoteza madhara yake ni makubwa na siyo rahisi kuirejesha.

 

Muungano

 

9. Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua za kutatua masuala ya Muungano yanayoleta kero kwa wananchi wetu wa pande zote kwa kufanya vikao mbalimbali. Kikao kimojawapo cha ngazi ya juu ni kile kilichoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kilichofanyika tarehe 15 Mei, 2008, Dar es Salaam. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kikao hicho kilijadili Taarifa za Utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa katika vikao viwili vya awali kati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Baadhi ya masuala yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kufungua Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora huko Unguja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuainisha miradi itakayoombewa ufadhili chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

10.  Mheshimiwa Spika, mbali na kikao cha Makamu wa Rais, vilifanyika pia vikao vingine 11 vya ushirikiano baina ya wizara mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar. Wizara zilizohusika na vikao hivyo ni pamoja na Mawasiliano, Uchukuzi na Miundombinu; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Maliasili na Utalii; Viwanda, Biashara na Masoko; Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Sheria, Katiba na Utawala Bora; Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Katika vikao hivyo, masuala mbalimbali yanayohusu sekta husika yalijadiliwa kwa maelewano na kufikiwa muafaka.

 

11. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia zimeridhia uteuzi wa Mshauri Mwelekezi atakayeshauri kuhusu mgawanyo wa mapato yatokanayo na rasilimali ya mafuta. Kazi hii inatarajiwa kukamilishwa mwezi Agosti, 2008 na kuwasilishwa katika Serikali zote mbili mwezi Septemba, 2008. Aidha, uandaaji wa kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu utakamilika mwezi Septemba, 2008.

 

12.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kutekeleza masuala yafuatayo:

 

a) Kuratibu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano katika vikao mbalimbali vikiwemo vya kimataifa;

 

b) Kuratibu, kuandaa na kushiriki katika vikao vya Makamu wa Rais na Mawaziri wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

 

c) Kufanya utafiti wa mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano;

 

d) Kutoa elimu kwa umma kuhusu mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano;

 

e)  Kuanisha maeneo ya uchumi katika nchi yetu ambayo yakitekelezwa yataleta faida kwa pande zote mbili; na

 

f) Kuratibu mgawanyo wa mapato ya pande zote mbili za Muungano.

 

Ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa karibu zaidi, vikao vya pamoja vitafanyika kila baada ya miezi miwili chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais.

 

 Chaguzi Ndogo

 

13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, nchi yetu ilifanya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kiteto na chaguzi ndogo za madiwani katika Kkata 16 Nchini. Katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kiteto, vyama vinne vya siasa vilishiriki. Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole-Nangoro, alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa kupata kura 21,506 sawa na asilimia 61 ya kura zote zilizopigwa. CHADEMA kilipata kura 12,561, SAU kura 300 na PPT Maendeleo kura 110. Kwa mara nyingine nampongeza Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole-Nangoro aliyeshinda uchaguzi huo. Uchaguzi huo pamoja na chaguzi ndogo mbalimbali za madiwani zilifanyika katika mazingira yaliyokuwa huru, amani na yaliyozingatia misingi bora ya demokrasia.

 

14. Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Agosti, 2007 Mheshimiwa Dk. Christine Gabriel Ishengoma (CCM) aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kujaza nafasi ya marehemu Amina Chifupa Mpakanjia. Mheshimiwa Mchungaji Dk. Getrude Pangalile Rwakatare (CCM) aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kuanzia tarehe 26 Novemba, 2007 kujaza nafasi ya marehemu Salome Joseph Mbatia. Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mheshimiwa Al-Shymaa John Kwegyir kuwa Mbunge wa Viti Maalum kuanzia tarehe 8 Aprili 2008. Wote nawapongeza sana kwa kuteuliwa kuwa Wabunge.

 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

 

15.  Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza awamu ya kwanza ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwaingiza wale waliotimiza sifa za kujiandikisha na kuwaondoa waliopoteza sifa. Hadi sasa, uboreshaji wa Daftari hilo umefanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Iringa, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Mwanza na Kagera. Zoezi hili litaendelea kwa mikoa ya Mara, Shinyanga, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar. Awamu ya Pili ya Uboreshaji wa Daftari hilo itafanyika mwaka 2009/2010 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2010. Lengo ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi aliye na sifa za kujiandikisha kuwa mpigakura anapatiwa nafasi hiyo ili aweze kushiriki katika uchaguzi huo.

 

Vyama vya Siasa

 

16.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilianza kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye madiwani. Vyama vinavyopata ruzuku hiyo ni CCM, TLP, CHADEMA, CUF, UDP na PPT-MAENDELEO. Kiasi cha shilingi bilioni 3 kilitengwa na Serikali kwa ajili ya ruzuku hiyo. Vilevile, Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa zilianza kutumika rasmi kupitia Tangazo la Serikali Na. 215 la tarehe 12 Oktoba, 2007. Wadau wote wamefahamishwa na kupatiwa nakala ya Kanuni hizo. Nachukua nafasi hii kuvishauri vyama vya siasa visome kwa makini, viheshimu na kuzifuata kanuni hizo, ili kuepuka migongano inayotokea kati ya vyama vyetu. Aidha, Serikali inafanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 kwa lengo la kuondoa migongano, migogoro na mahusiano mabaya ndani ya vyama vya siasa. Marekebisho hayo yatawasilishwa hapa Bungeni katika Mkutano wa Bunge wa Kumi na Tatu mwezi Novemba 2008.

 

17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, usajili wa muda wa vyama viwili ulifutwa baada ya kupoteza sifa za usajili wa muda na kushindwa kutimiza masharti ya maombi ya usajili wa kudumu. Vyama hivyo ni Tanzania Peoples Organisation for Democracy and Development (TAPODD) ambacho kilifutwa tarehe 31 Julai, 2007 na National Progressive Democratic Party (NPDP) kilichofutwa tarehe 16 Aprili, 2008. Aidha, Serikali ilitoa elimu ya uraia kuhusu faida na majukumu ya kila taasisi na mwananchi katika mfumo wa demokrasia kwa vyama vya siasa.

 

Shughuli za Bunge

 

18.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Bunge lako tukufu limeendelea kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba ya kutunga sheria na kuishauri Serikali. Mabadiliko ya Kanuni za Bunge yalifanyika ambapo Kamati za Kudumu za Bunge zilizopo sasa zinawawezesha Waheshimiwa Wabunge kuchambua kikamilifu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na kusimamia shughuli za utendaji wa Serikali kwa umakini zaidi.Aidha,Bunge lako tukufu lilipitisha Miswada ya Sheria 24, liliridhia Maazimio 14 yanayohusu masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa na maswali ya msingi 970 yaliulizwa na kupatiwa majibu. Vilevile, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumuuliza Waziri Mkuu maswali ya papo kwa papo Bungeni. Katika mwaka 2008/2009, Ofisi ya Bunge itaendelea kusimamia mipango ya mafunzo kwa watendaji, kuendeleza mahusiano na mabunge ya nchi nyingine na kuboresha huduma mbalimbali za kiutawala na elimu kwa wabunge.

 

Ofisi za Wabunge 

 

19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilitenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Wabunge. Jumla ya majimbo 40, yakiwemo 32 ya Tanzania Bara na 8 ya Tanzania Visiwani yaliteuliwa kupata fedha za ujenzi wa ofisi hizo katika awamu ya kwanza. Hata hivyo, kutokana na ongezeko la gharama, mchanganuo wa kitaalam unaonyesha kuwa gharama halisi za ujenzi wa ofisi moja iliongezeka kutoka shilingi milioni 25 zilizokuwa zimekadiriwa awali hadi shilingi milioni 40. Katika mwaka 2008/2009, Serikali imetenga shilingi bilioni moja ili kukamilisha ujenzi wa ofisi 40 katika awamu ya kwanza na kuanza ofisi 10 za awamu ya pili. Suala hili litasimamiwa kikamilifu na Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Kiongozi ili kuona lengo hilo linafikiwa.

 

HALI YA UCHUMI

 

20.  Mheshimiwa Spika, mwenendo wa hali ya uchumi wetu kwa ujumla unaridhisha. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Uchumi, katika mwaka 2007 uchumi wetu ulikua kwa asilimia 7.1, licha ya kuwepo kwa misukosuko mbalimbali ya kiuchumi. Mfumuko wa Bei, ambao ulifikia asilimia 9 mwezi Machi 2008, umeendelea kuwa juu kufuatia kupanda kwa bei ya nafaka, mafuta ya petroli pamoja na bidhaa nyingine kutoka nje. Wataalam wa uchumi duniani wanaeleza kuwa matarajio ya mwenendo wa bei za bidhaa katika Soko la Dunia hususan bei za nishati na nafaka kwa mwaka ujao zitaendelea kupanda.

 

21.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaweka mazingira mazuri yatakayowezesha sekta zote kukua kwa kasi inayoridhisha ili kufikia lengo tulilojiwekea la ukuaji halisi wa Pato la Taifa la asilimia 7.8. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi ni endelevu na wa viwango vikubwa kati ya asilimia 8 hadi 10. Viwango hivyo ndivyo vitakavyoboresha na kuendeleza huduma za jamii na kiuchumi na hatimaye kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa. Hivyo, sote tuongeze matumizi bora ya rasilimali zilizopo na jitihada zaidi zielekezwe kuongeza tija katika sekta za kilimo, miundombinu, madini na huduma za kijamii. Aidha, juhudi zielekezwe katika utoaji wa mikopo midogo ili kujenga na kuendeleza ujasiriamali kwa mtu mmoja mmoja au vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na utoaji huduma.

 

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

 

22.  Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2006/2007, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuwashirikisha wananchi wengi zaidi katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Serikali ilitenga shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mpango huo ambapo Benki za CRDB na NMB ziliteuliwa kushiriki katika utekelezaji na ziliafiki kutoa mkopo mara tatu ya kiwango cha dhamana kilichokubalika kwa kutumia mitaji yao wenyewe. Katika awamu ya kwanza ya mpango huo, Benki hizo ziliweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 32.7 kwa wajasiriamali 44,256. Kutokana na mafanikio hayo, awamu ya pili ya utoaji mikopo kwa wajasiriamali ilizinduliwa mwezi Desemba 2007. Jumla ya asasi za kifedha 14 zilijitokeza kushiriki kwenye mpango huo ili kukopesha shilingi bilioni 10.5 zilizotengwa katika awamu ya pili. Hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 3.7 zimetolewa katika asasi hizo za fedha. Kati ya hizo, shilingi milioni 881.3 zimekopeshwa kwenye Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) mbalimbali hapa nchini. Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipatiwa shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi  wananchi wa Tanzania Visiwani.

 

23. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi umeonyesha mafanikio na changamoto kadhaa. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuwepo na ongezeko kubwa la mwamko wa wananchi kutumia huduma za kibenki na ari kubwa miongoni mwao kuhusu faida za kujiunga na SACCOS.Hii imetokana na jitihada za uhamasishaji kupitia kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali wa kitaifa, mikoa, wilaya na vijiji.Aidha, mpango huo umehamasisha na kuendeleza dhana ya wananchi kujiajiri kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayobuniwa na mtu mmoja mmoja au vikundi. Kutokana na uhamasishaji huo, miradi mingi mipya ya kiuchumi imeanzishwa na ile iliyokuwa inalegalega imefufuliwa hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.

 

24. Mheshimiwa Spika, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na wananchi wengi kujitokeza kuomba mikopo ikilinganishwa na kiasi kidogo cha fedha kilichotengwa. Changamoto nyingine ni wananchi wengi kutokuwa na elimu ya ujasiriamali inayowawezesha kubuni na kuandaa miradi mizuri inayokopesheka, kuiendesha kwa ufanisi pamoja na kupanga matumizi bora ya mikopo waliyokopeshwa na urejeshaji wake.Aidha, katika awamu ya kwanza ipo mikoa ambayo ilipata mgao wa fedha za mikopo chini ya kiwango cha shilingi milioni 500. Pia, zipo wilaya 21 ambazo hazikupata kabisa mikopo katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa matawi ya Benki za CRDB na NMB.Hata hivyo, baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zimetafutiwa ufumbuzi wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili. Eneo muhimu lililoshughulikiwa ni lile la kuhakikisha kuwa mikoa, wilaya na maeneo ambayo hayakunufaika na mpango huu katika awamu ya kwanza yanapewa kipaumbele. Katika mwaka 2008/2009, Serikali itaboresha zaidi utekelezaji wa mpango huu ili uwe na tija kubwa. Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza  wananchi kote nchini kuendelea kujiunga na SACCOS ili waweze kunufaika na mpango huu.

 

Kituo cha Uwekezaji Tanzania

 

25. Mheshimiwa Spika, jitihada za kutangaza vivutio vyetu zimewezesha kuongezeka kwa miradi inayowekezwa na wawekezaji mbalimbali hapa nchini. Katika mwaka 2007/2008, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili jumla ya miradi 902 yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.1 ambayo imetoa ajira zipatazo 127,588. Kati ya miradi hiyo, miradi 483 ni ya Watanzania, 196 ni ya wageni na 223 ni ya ubia. Takwimu za kimkoa zinaonyesha kwamba mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kusajili miradi 502, Arusha miradi 158, Mwanza 51, Kilimanjaro 32 na Pwani 31. Mikoa mingine ni Shinyanga miradi 17, Morogoro 16, Mbeya 15, Tanga 14, Iringa 13, Kagera 12, Dodoma 11, Mara 9, Lindi 6, Mtwara 4, Tabora 4, Singida 2, Manyara 3, Rukwa 3, Ruvuma 1 na Kigoma 1. Sekta ya utalii ndiyo iliyoongoza kupata miradi mingi kwa kusajili miradi 275 ikifuatiwa na sekta ya viwanda yenye miradi 236 na sekta za nyumba na biashara ina miradi 125.

 

26.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kitaendelea kuitangaza nchi yetu kwa kutumia mitandao ya kimataifa; kuwaunganisha wawekezaji wadogo na wawekezaji wenye viwanda vikubwa hapa nchini ili waweze kushirikiana kibiashara na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kukuza biashara zao. Natoa wito kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kutumia huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania ili waweze kujiendeleza kibiashara. Kituo hiki hakipo kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa nje tu bali ni kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza mitaji yao hapa nchini. Aidha, mikoa itangaze vivutio na fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo tovuti na mikutano ya wafanyabiashara popote pale itakapofanyika.

 

Uimarishaji wa Sekta Binafsi

 

27.  Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Ili kupunguza vikwazo ambavyo sekta binafsi inakumbana navyo kama vile ukosefu wa fedha za kutosha za uwekezaji, kutokuwa na taarifa sahihi za masoko ya bidhaa za nje na teknolojia duni, Serikali imetoa udhamini wa mkopo wa dola za Marekani milioni 16 kutoka Benki ya Dunia kwa taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania. Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 6 zitatumika kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na wa kati. Chini ya mpango huo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania itatoa asilimia 50 ya mtaji wa biashara inayokusudiwa kuendeshwa na wafanyabiashara watachangia asilimia 50 iliyobakia. Sehemu nyingine ya fedha hizo, kiasi cha dola za Marekani milioni 10 kitatumika kuviongezea uwezo vyuo na taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi ili viweze kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuandaa mipango ya biashara inayouzika. Natoa wito kwa wafanyabiashara kuchangamkia mikopo hii ili iwasaidie kukabiliana na vikwazo vinavyowazuia kufanya shughuli zao kwa ufanisi. Vilevile, taasisi na vyuo vya ufundi vitakavyonufaika na mpango huu vihakikishe kwamba mafunzo yatakayotolewa yatawasaidia wajasiriamali kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

 

Baraza la Taifa la Biashara

 

28. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara ni chombo kinachounganisha Sekta Binafsi na Sekta ya Umma kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Tanzania. Katika mwaka 2007/2008, Baraza liliendelea kuimarisha majadiliano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ili iwe mhimili mkuu wa uchumi. Majadiliano hayo yalilenga kuboresha mazingira ya kuendesha biashara na uwekezaji. Aidha, jumla ya Mabaraza ya Biashara ya Mikoa 21 yameundwa Tanzania Bara na jitihada za kuanzisha Mabaraza ya Biashara ya Wilaya zimeanza. Madhumuni ya mabaraza haya ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji na kuibua fursa za uwezeshaji kiuchumi katika ngazi za chini.

 

29. Mheshimiwa Spika, vilevile, Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi liliandaa midahalo mbalimbali ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi nchi nzima. Madhumuni ya midahalo hiyo ilikuwa ni kuainisha maoni na uelewa wa dhana nzima ya uwekezaji toka kwa wananchi na jinsi wanavyoweza kuibua miradi ya kuwaongezea kipato na hivyo kuwa na maisha bora. Midahalo ilifanyika katika ngazi ya wilaya na mikoa na hatimaye Mdahalo wa Kitaifa utafanyika mara baada ya majadiliano ya Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Matokeo ya mdahalo huo yatafikishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara kwa madhumuni ya kupanga utekelezaji.

 

30.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Baraza la Taifa la Biashara, litafanya mkutano wake wa tano utakaohusisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana mawazo na uzoefu wa jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Aidha, Baraza litasimamia na kuimarisha shughuli za Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya pamoja na shughuli za vikundi kazi vikuu vilivyoanzishwa na Baraza vya kuboresha Kilimo, Kukuza Viwanda na Mauzo ya Nje, Ardhi, Utalii, Rasilimali Watu, Huduma za Fedha, Miundombinu na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

 

Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo

 

31.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali kupitia Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo imewezesha kuundwa na kuimarishwa kwa vikundi vya wazalishaji, wafanyabiashara na wasindikaji wadogo vipatavyo 232 katika wilaya tisa za Chunya, Ileje, Kyela, Makete, Njombe, Korogwe, Simanjiro, Mwanga na Moshi Vijijini. Vikundi hivyo vimejengewa uwezo kwa njia ya mafunzo ya mbinu mbalimbali za kutafuta masoko na kuviunganisha na masoko ya mazao yao. Aidha, vikundi 1,076 vimepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uongozi, biashara, uchaguzi wa mazao ya biashara, utafiti shirikishi wa masoko, ukokotoaji wa gharama na masuala mtambuka, yakiwemo ya jinsia, UKIMWI na mazingira.

 

32. Mheshimiwa Spika, ili kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa Wakulima, Programu imehamasisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani. Chini ya Mfumo huu, wakulima huhifadhi mazao ghalani na kupewa stakabadhi ambazo wanaweza kuzitumia kama dhamana kwamikopo watakayoiomba benki na kurejesha mkopo huo baada ya kuuza mazao yao wakati bei ikiwa nzuri. Utekelezaji wa mfumo huo umefanyika katika maghala manane katika wilaya za Hanang (2), Mbarali (2), Songea, Mbozi, Mufindi na Sumbawanga Vijijini. Wakulima 879 wamepatiwa mikopo ya thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa kutumia mfumo huu.

 

33. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Programu hii imekarabati barabara za Vijijini zenye urefu wa Kilomita 670 ili kuboresha miundombinu inayohusiana na masoko ya mazao ya kilimo na kurahisisha muingiliano baina ya Wazalishaji, Wasindikaji na Wafanyabiashara Vijijini. Aidha, jumla ya masoko 14 yamejengwa na yamekamilika. Masoko hayo ni Kikatiti (Arumeru), Kwa Sadala (Hai), Inyala (Mbeya), Gallapo (Babati), Katesh (Hanang), Monduli (Monduli) na Matai (Sumbawanga Vijijini). Masoko mengine yaliyokamilika ni ya Tarakea (Rombo), Kiwira (Rungwe), Soni (Lushoto), Tunduma (Mbozi), Makita (Mbinga), Mlangali (Ludewa) na Mtindiro (Muheza). Masoko ya Hedaru (Same), Kinyanambo (Mufindi) na Dongobesh (Mbulu) yapo katika hatua za mwisho za kukamilishwa ujenzi.

 

34.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kuimarisha vikundi vya wazalishaji, wafanyabiashara na wasindikaji wadogo. Aidha, itaanza utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwenye maeneo ambayo yameonyesha kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ya Kirando (Nkasi), Ipinda (Kyela), Majimoto  (Mpanda), Mpitimbi  (Songea  Vijijini), Monduli (Monduli) na Bashay (Mbulu). Vilevile, jumla ya kilomita 323.6 za barabara zitakarabatiwa na masoko 7 yatajengwa katika wilaya za Chunya, Ileje, Kyela, Makete, Njombe, Korogwe na Simanjiro.

 

Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini

 

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali chini ya Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini, imefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kipato kwa  wananchi wanaoishi vijijini. Kwa kutumia mbinu shirikishi na mafunzo kwa wanachama wa SACCOS, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanachama, hisa, amana na  akiba. Aidha, ushiriki wa wanawake umeongezeka ikiwa ni pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali katika Asasi hizo. Programu pia imeimarisha Benki za  wananchi za Mwanga, Mufindi na Mbinga na Benki ya Ushirika Kilimanjaro kwa kuzipatia magari, kutoa mafunzo kwa watumishi na kuimarisha usimamizi wa mifumo ya fedha.

 

36.  Mheshimiwa Spika, Programu ilitoa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati za Mikopo na Maafisa wa Mikopo 1,100 wa SACCOS 276. Mafunzo hayo yaliwawezesha kuelewa masuala ya Dhana, Kanuni, Misingi na Taratibu za kutoa mikopo pamoja na kusimamia na kuhakikisha mikopo inarejeshwa. Aidha, Vikao vya pamoja kati ya Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya za Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songea, Dodoma, Singida na Kilimanjaro viliitishwa kuzungumzia jinsi Wilaya zitakavyochukua hatamu za utekelezaji wa shughuli za kukuza na kuendeleza Asasi za Fedha Vijijini baada ya Programu kumaliza muda wake. Vilevile, Wahasibu 276 pamoja na Viongozi 100 walipewa mafunzo ya SACCOS.

 

37. Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2008/2009, Programu itaboresha usimamizi na utendaji wa Asasi Ndogo za Kifedha, kuimarisha mifumo ya kifedha Vijijini na kuwajengea uwezo  wananchi wa Vijijini ili waweze kujiunga na kushiriki katika shughuli za SACCOS. Aidha, Programu itaendelea kuimarisha Benki za  wananchi na kusaidia mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya  wananchi Njombe

 

38. Mheshimiwa Spika, Programu hizi zimekuwa zikisaidia juhudi za Serikali za kuondoa umaskini kwa kuwawezesha  wananchi wa vijijini kuongeza kipato kwa kupata huduma za mikopo kupitia Asasi za Kifedha na masoko ya uhakika ya mazao yao. Kutokana na utekelezaji wa Programu hizi mbili, uzoefu uliopatikana umebaini kuwepo kwa mafanikio makubwa katika Wilaya ambazo Programu hizi zinatekelezwa. Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la asasi za kifedha, wanachama na mitaji. Aidha, kwa kuimarisha Benki za wananchi, SACCOS nyingi zimeweza kupata mikopo kutoka katika Benki hizo ambayo imewekezwa katika miradi mbalimbali ya uzalishaji. Eneo jingine lililoonyesha mafanikio ni lile la kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani. Kupitia mfumo huu,  wananchi wengi wameweza kupata mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kueneza uzoefu huo tuliopata katika wilaya zote nchini. Ninazisihi Halmashauri za Wilaya hususan zile za jirani kutembelea Halmashauri ambazo zinatekeleza programu hizo kwa lengo la kuona na kujifunza mafanikio yaliyopatikana na baadaye kuyatekeleza katika Halmashauri zao.

 

Huduma za Kiuchumi

 

Barabara Kuu na za Mikoa

 

39. Mheshimiwa Spika, maendeleo ya uchumi wa Nchi yoyote ile hutegemea sana mtandao mzuri wa barabara. Barabara husaidia shughuli za kiuchumi na kijamii kustawi, kushamiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na mapato ya watu. Katika mwaka 2007/2008, Serikali ilikamilisha ujenzi wa barabara za Isuna - Singida (Km. 63), Singida - Shelui (Km. 110), Geita – Buzirayombo (Km. 100), Kyamiorwa - Buzirayombo (Km. 120), Nangurukuru – Mbwemkuru (Km. 95), Mbwemkuru – Mingoyo (Km. 95), Mkuranga – Kibiti (Km. 79) na Tarakea - Rongai – Kamwanga (Km. 32). Jumla ya kilomita 330.4 zilifanyiwa matengenezo ya muda maalum na kilomita 79.0 zilifanyiwa matengenezo katika sehemu korofi. Aidha, jumla ya madaraja na makalvati yapatayo 492 yamefanyiwa matengenezo ya kawaida katika barabara kuu na barabara za mikoa.

 

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara kuu. Baadhi ya Barabara hizo ni Manyoni - Isuna (Km. 54), Mbeya - Lwanjilo (Km. 36), Nelson Mandela (Km. 15.6), Kurasini – Mbagala (Km. 11.6) Masasi - Mangaka (Km. 54), Usagara – Sengerema - Geita (Km. 90) na Mwandiga – Manyovu (Km. 60). Aidha, kwa kupitia msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Millennium Challenge Corporation (MCC), Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za Tunduma – Sumbawanga (Km. 224.5), Songea – Namtumbo (Km. 70), Peramiho – Mbinga (Km. 80), Tanga – Horohoro (Km. 65), na kukarabati uwanja wa ndege wa Mafia.

 

Barabara za Vijijini

 

41.Mheshimiwa Spika, barabara za vijijini ni muhimu katika kuwasaidia  wananchi wanaoishi vijijini hasa wakulima kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye masoko. Ili kufikia azma hiyo, katika mwaka 2007/2008, Serikali za Mitaa zilitengewa jumla ya Shilingi bilioni 65 kutoka katika Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 37,229. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2008 kiasi cha shilingi bilioni 48.2 kilikuwa kimepelekwa kwenye Halmashauri na kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 7,592 yakiwemo matengenezo ya kawaida kilomita 4,988, matengenezo madogo madogo kilomita 2,099, matengenezo ya muda maalum kilomita 505 pamoja na matengenezo ya madaraja na makalvati.

 

42. Mheshimiwa Spika, kupitia Programu ya Usafiri katika Serikali za Mitaa, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya ukarabati wa barabara. Hadi kufikia mwezi Aprili 2008 kiasi cha shilingi bilioni 5.8 kilikuwa kimepelekwa kwenye Halmashauri zote nchini kusaidia kuboresha kilomita 1,000 za maeneo korofi. Aidha, Serikali iliendelea kutekeleza Programu ya Usafiri na Uchukuzi Vijijini. Programu hii ilitumia jumla ya shilingi bilioni 1.9 katika Halmashauri 27 ili kufanya matengenezo ya barabara za jamii, ujenzi wa madaraja madogo na kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu matumizi bora ya teknolojia rahisi.

 

43.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaendelea kufanyamatengenezo ya barabara katika Serikali za Mitaa. Jumla ya Shilingi bilioni 65 kutoka kwenye Mfuko wa Barabara zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Vijijini. Aidha,kupitiaProgramu ya Usafiri katika Serikali za Mitaa, jumla ya Shilingi bilioni 16.8 zitapelekwa katika Halmashauri kwa ajili ya matengenezo ya barabara, maeneo korofi, madaraja na uwekaji wa makalvati. Programu ya Usafiri na Uchukuzi Vijijini imetengewa shilingi bilioni 1.8 ili kuboresha usafiri vijijini katika Halmashauri 55. Fedha hizi zikisimamiwa vizuri barabara nyingi za vijijini zitaimarika na kupitika kwa wakati wote.

 

Usafiri Katika Jiji la Dar es Salaam

 

44.  Mheshimiwa Spika, Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo kubwa la usafiri na usafirishaji kutokana na ongezeko la watu na magari. Katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na maboresho ya barabara zinazoingia na kutoka barabara kuu na kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani. Pamojana hatua hizo, Serikali imekamilishamaandalizi ya Mpango Kamambe wa Usafirishaji kwa Jiji la Dar es Salaam. Mpango huu umeainisha kwa kina mikakati ya muda wa kati na mrefu wa kuondoa kero ya usafiri na msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, napenda kusisitiza kuwa, wakati mwingine msongamano wa magari unatokana na uendeshaji wa kibabe. Hivyo, natoa wito kwa madereva wote kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani na askari wa usalama barabarani wasimamie kikamilifu Sheria hiyo. Aidha, adhabu kali zaidi zitolewe kwa wale watakaokiuka Sheria hiyo.

 

45. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Jijini Dar es Salaam (Dar es Salaam Rapid Transport-DART) unaendelea vizuri. Usanifu wa kina utakaowezesha kujengwa kwa miundombinu inayokidhi watumiaji wote wa barabara na matumizi ya mabasi yenye  ujazo  mkubwa  wa  kupakia  abiria  umekamilika. Jumla ya gharama za mradi huu katika awamu ya kwanza ni dola za Marekani milioni 158.2. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania itatoa dola za Marekani milioni 10, Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 110 na Sekta Binafsi itawekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 38.2 kwa kununua mabasi na kujenga mfumo imara wa kukusanya nauli. Awamu ya Kwanza ina urefu wa kilometa 21 na ina vituo vidogo 29, vituo vikubwa 5 na maeneo mawili ya maegesho na matengenezo. Fidia kwa  wananchi ambao mali zao zinaathiriwa na ujenzi wa miundombinu ya DART zinaendelea kulipwa na zoezi hilo litakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2008. Ujenzi wa miundombinu utaanza katika mwaka 2008/2009 na inategemewa utachukua muda wa miezi 24.

 

Vivuko

 

46.Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha huduma ya Vivuko Nchini kwa kununua Vivuko vipya na kukarabati vilivyopo. Vivuko vipya vilivyonunuliwa ni vya Kigongo – Busisi chenye uwezo wa kubeba tani 250, kivuko cha Kilombero chenye uwezo wa kubeba tani 50 na Kivuko cha Kigamboni chenye uwezo wa kubeba tani 500. Aidha, Serikali imenunua kivuko cha Ruhuhu chenye uwezo wa kubeba tani 50 kwa ajili ya  wananchi wa Wilaya za Mbinga na Ludewa. Katika mwaka 2008/2009, kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 40 kitakachotoa huduma kati ya Nyakalilo na kisiwa cha Kome kitanunuliwa na kivuko kipya cha Pangani chenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 50 kinaendelea kuundwa. Vilevile, vivuko vya M.V. Alina cha Dar es Salaam na Rugezi - Kisorya vimefanyiwa matengenezo.

 

Nishati

 

47.              Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mipango ya usambazaji wa Umeme kwa  wananchi Mijini na Vijijini. Katika mwaka 2007/2008, Serikali imeipatia TANESCO fedha za kununua mitambo mipya ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya dizeli yenye uwezo wa kuzalisha KVA 1,200 kwa ajili ya mji wa Mbinga. TANESCO pia imekamilisha kazi ya kuweka nyaya za kusambaza umeme katika mji wa Ludewa. Aidha, kwa kutumia fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini, Wakala wa Nishati Vijijini ilifanya upembuzi yakinifu katika maeneo ya Kilolo, Mbinga, Mto wa mbu, Bahi, Uyui, Mkinga, Simanjiro na Kilindi. Serikali pia imekamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi wa North- West Grid Studyunaojumuisha Mikoa ya Kigoma, Kagera na Rukwa. Vilevile, shughuli za Mradi wa Uendelezaji Huduma za Nishati Vijijini unaohamasisha Soko la Umemenuru zimezinduliwa katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Kigoma, Pwani, Rukwa na Mtwara.

 

48.             Mheshimiwa Spika, Sekta ya Nishati pia itafaidika na msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Millennium Challenge Corporation (MCC). Kiasi cha dola za Marekani milioni 206 kutoka MCC kitatumika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro, Dodoma na Tanga. Vilevile, kiasi cha dola za Marekani milioni 63.1 kitatumika katika ujenzi wa njia ya umeme wa chini ya maji kwenda Zanzibar. Aidha, kiasi cha Dola za Marekani milioni 53.7 kitatumika kuzalisha umeme wa megawati 8 kutokana na nguvu za maji katika mto Malagarasi.

 

49.              Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga Fungu. Mradi huu utanufaisha maeneo ya Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Somanga, Kibiti na maeneo mengine ya jirani. Serikali pia itakamilisha uwekaji umeme katika maeneo ya Kilolo, Mbinga, Mto wa Mbu, Bahi, Uyui, Mkinga, Simanjiro na Kilindi. Aidha, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, Serikali itaongeza kasi ya usambazaji wa Nishati Vijijini chini ya Mradi wa Uendelezaji na Kupanua Wigo wa Upatikanaji na Usambazaji wa Nishati Nchini.

 

Mawasiliano

 

50.             Mheshimiwa Spika, shughuli nyingi katika Sekta ya Mawasiliano zinaongozwa na Sekta Binafsi ambazo kwa ujumla zimeonyesha mafanikio makubwa. Kampuni za Simu za Mkononi zimepanua huduma za mitandao yao hadi Vijijini na hivyo kuwaongezea Watanzania wigo wa mawasiliano. Takwimu zinaonyesha kwamba Wateja wa simu za mkononi wameongezeka kutoka milioni 5.7 mwaka 2006 hadi milioni 8.5 mwaka 2007. Hii ni dalili njema kwani mawasiliano ni kichocheo muhimu cha biashara na hupunguza ulazima wa safari kutoka eneo moja kwenda jingine na hivyo kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi. Miundombinu ya huduma za utangazaji pia iliboreshwa na matokeo yake ni kupanuka kwa maeneo yanayofikiwa na huduma za utangazaji unaotolewa kwa njia za Redio na Luninga na hivyo kuwafikia  wananchi wengi hususan waishio Vijijini.

 

51.             Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na mchakato wa kuunda Mfuko wa Mawasiliano Vijijini. Mfuko huu utasaidia kufikisha huduma za mawasiliano Vijijini kwa kuwapatia ruzuku wawekezaji walio tayari kupeleka miundombinu na huduma za mawasiliano sehemu zote ambazo hazina mvuto wa kibiashara. Vilevile, Serikali iliendelea kuimarisha vituo vya Mawasiliano Nchini vikiwemo vya Dar es Salaam, Sengerema, Mpwapwa, Kasulu, Mtwara, Kinampanda mkoani Singida na Wino mkoani Ruvuma kwa ajili ya wakulima wa Kahawa. Vituo hivyo vitatumiwa na jamii katika kukuza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ajili ya biashara, masomo, afya na utawala.

 

52.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali itaanza utekelezaji wa awali wa ujenzi na uendelezaji wa Mkongo wa Kitaifa wa Mawasiliano na kuratibu uanzishwaji wa mfumo mpya wa anuani na namba za posta nchini ili kurahisisha na kuboresha huduma zitolewazo na sekta nyingine. Aidha, vituo zaidi vya mawasiliano vitaanzishwa katika mikoa mingine kwa lengo la kuwafikia  wananchi wengi hususan makundi ya wasiojiweza, wanawake na wengine waishio sehemu za vijijini. Vituo hivyo vitawawezesha  wananchi kupata habari muhimu za kijamii na kiuchumi.

 

Ardhi

 

53.             Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kwamba ardhi ni rasilimali ya msingi kwa maendeleo ya Taifa letu na ni tegemeo  kubwa la wananchi wengi kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara. Ardhi ikigawanywa na kutumiwa bila utaratibu unaokubalika na jamii huwa chanzo kikubwa cha migogoro ya mipaka. Kwa upande mwingine, ardhi ikitumiwa holela husababisha uharibufu wa mazingira, mmomonyoko wa ardhi na hivyo kupunguza rutuba ya ardhi na hatimaye Nchi kuwa jangwa. Hivyo, Serikali ina wajibu wa kuhakikisha ardhi yetu, ambayo haiongezeki, inatumiwa kwa busara ili iweze kuendelea kuwa rasilimali endelevu kwa maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo.

 

54.             Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumeshuhudia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayosababishwa na jamii za Wakulima na Wafugaji kugombea maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na maendeleo. Aidha kumekuwepo na migogoro ya mipaka kati ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji. Serikali imebaini kuwa sababu kuu za migogoro hiyo ni pamoja na kung’olewa au kupotea kwa alama za mipaka na ukuaji holela wa Vijiji kiasi cha kuingilia maeneo mengine ya kiutawala kama vile maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa au hifadhi ya vyanzo vya maji. Vilevile, kumekuwepo na ufahamu mdogo wa baadhi ya  wananchi na watendaji juu ya mipaka ya maeneo yao ya kiutawala kutokana na ukweli kwamba, maelezo ya mipaka yaliwekwa miaka mingi iliyopita. Katika maeneo ya Mijini kumekuwa na ukiukwaji wa Sheria na Taratibu za Mipango Miji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bila vibali vya Mamlaka ya Miji husika.

 

55.             Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na matatizo hayo ya ardhi, katika mwaka 1995, Serikali iliandaa Sera ya Ardhi ambayo utekelezaji wake ulianza kwa kutunga sheria mbalimbali. Maudhui ya Sheria hizo ni kutoa maelekezo ya Taratibu na Kanuni za umiliki na matumizi endelevu ya ardhi yetu. Maandalizi ya Sera na Sheria hizi yalishirikisha Wadau wengi na yamezingatia mabadiliko ya kiuchumi na mahitaji ya utandawazi. Sheria hizo zimeanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuunda Vyombo vya Usimamizi wa utekelezaji wake. Vyombo hivyo ni pamoja na Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na Mabaraza ya Ardhi. Tume ina jukumu la kusimamia utayarishaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi na Mabaraza ya Ardhi yanashughulikia Mashauri ya migogoro ya ardhi.

 

56.             Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ikitekeleza majukumu yake ya kupanga matumizi bora ya ardhi ipasavyo katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya, Miji na Vijiji, itazuia kwa kiasi kikubwa kutokea migogoro ya ardhi Nchini. Vilevile, Mabaraza ya Ardhi yakifanya kazi zake kwa ufanisi yataharakisha uamuzi wa Mashauri ya Ardhi na hivyo kuendeleza amani Nchini. Hali hii itawavutia Wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika mashamba ya biashara, viwanda na mahoteli katika maeneo ambayo yametengwa na kupimwa kwa shughuli hizo.

 

57.             Mheshimiwa Spika, uzoefu uliopatikana katika zoezi la kuwahamisha Wafugaji na mifugo yao kutoka Bonde la Ihefu umedhihirisha umuhimu wa kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Serikali za Mitaa na Vijiji. Katika zoezi hilo, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Serikali za Vijiji iliweza kuainisha maeneo ya kutosha ya kuhamishia mifugo katika Wilaya za Kisarawe, Rufiji, Lindi, Nachingwea na Kilwa. Maeneo hayo ya malisho yaliweza kupatikana baada ya Halmashauri hizo kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Wilaya zao.

 

58.             Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mafanikio yaliyopatikana katika utaratibu Shirikishi wa kutayarisha Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi chini ya uratibu wa Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi;naelekeza kwamba, kila mwaka Halmashauri zitenge fedha za kutosha kwa ajili ya utayarishaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Zoezi hili liende sambamba na upimaji wa viwanja mijini na mashamba makubwa ya kilimo na ufugaji. Aidha, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi itaimarishwa ili kuiwezesha kuratibu utayarishaji na usimamizi wa utekelezaji wa mipango hiyo muhimu. Lengo ni kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa  kila  Halmashauri  na  kila Kijiji na Miji yote. Zoezi hili liende sambamba na uboreshaji wa Kumbukumbu za Ardhi na ujenzi wa Masjala za Ardhi katika ngazi za Wilaya na Vijiji ili kupunguza migogoro ya miliki za Viwanja na mashamba.

 

59.             Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kutoa rai kwa  wananchi na Viongozi wa ngazi zote kutoa ushirikiano katika utatuzi wa migogoro ya ardhi. Katika kusuluhisha migogoro hiyo, ni vyema tukajenga utamaduni wa kukaa kwa pamoja na kumaliza matatizo kabla hayajawa makubwa na kuleta athari kwa  wananchi. Vilevile, napenda kutoa tahadhari kwa  wananchi ambao wanavamia ardhi iliyokwishapimwa na kuendeleza makazi na kudai fidia pale wanapoondolewa Kisheria. Serikali haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria na taratibu za nchi na haitasita kuwachukulia hatua za nidhamu mara moja watumishi watakaobainika kutokuwa waadilifu katika utoaji wa huduma za ardhi.

 

SEKTA YA UZALISHAJI MALI

 

Kilimo

 

60.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/2008, Serikali ilipanga kutoa mbolea ya ruzuku kiasi cha Tani 89,820. Hadi kufikia mwezi Mei 2008 tani 74,503, sawa na asilimia 83 ya lengo zilikuwa zimesambazwa. Vilevile, jumla ya Tani 3,222 na Lita 133,463 za dawa ya korosho zilisambazwa kwa utaratibu wa ruzuku. Bodi ya Pamba ilinunua na kusambaza dawa za kuulia wadudu aina ya acrepacks 500,000 zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4. Aidha, jumla ya Makampuni 12 yalisaini Mkataba na Serikali wa kusambaza Tani 1,770 za mbegu za Mazao ya Mahindi, Mtama na Alizeti. Hadi mwezi Aprili 2008, jumla ya Tani 1,170 za mbegu sawa na asilimia 66 zilifikishwa katika vituo 21 vya usambazaji Mikoani ambapo Tani 969 zimeuzwa kwa Wakulima. Kwa upande wa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo, hadi kufikia mwezi Mei 2008, jumla ya Shilingi bilioni 3.1 kati ya Shilingi bilioni 3.5 zilizotengwa zimetolewa kwa ajili ya kutoa mikopo.

 

61.             Mheshimiwa Spika, ili kuongeza tija katika kilimo, hatua kabambe zitakazowezesha ongezeko la uzalishaji katika Sekta hiyo inabidi zichukuliwe. Hatua ya kwanza itakuwa ni kuhakikisha kwamba Wakulima wanapata mbolea nyingi kwa msimu ujao wa kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji. Ili Wakulima wapate mbolea hiyo kwa wakati na kwa gharama nafuu, katika mwaka wa fedha 2008/2009, Serikali itatoa dhamana kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania ili iweze kununua na kusambaza tani 150,000 za mbolea ya kupandia itakayozalishwa na Kiwanda cha Minjingu kabla ya msimu wa mvua kuanza. Aidha, itaongeza fedha za ruzuku kwa ajili ya usafirishaji wa mbolea ili kuwezesha vyombo vitakavyosafirisha mbolea yote inayozalishwa Minjingu pamoja na ile itakayoagizwa kutoka nje kusafirishwa na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.

 

62.             Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Juni, 2008 nilitembelea Kiwanda cha Mbolea Minjingu. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kiwanda hicho ili kubainisha mahitaji ya msingi ya muda mfupi na mrefu ambayo Serikali inaweza kuyatafutia ufumbuzi ili kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha mbolea nyingi zaidi. Aidha, nilitaka kujiridhisha kama kiwanda hiki kina uwezo wa kutengeneza mbolea ya kutosha ambayo kwa sasa tunaihitaji sana kutokana na unafuu wa bei ikilinganishwa na mbolea zinazoagizwa kutoka nje. Nimehakikishiwa na uongozi wa Kiwanda cha Minjingu kwamba kina uwezo wa kuzalisha mbolea ya Phosphate kati ya tani 150,000 hadi 200,000 kwa mwaka.

 

63.             Mheshimiwa Spika, Serikali itakiwezesha Kiwanda cha Mbolea Minjingu kuagiza nje virutubisho maalum kama Sulphur, Nitrogen Potassium, Zinc na Copper ili viongezwe kwenye mbolea ya chengachenga inayozalishwa na kiwanda hicho. Hatua hii itaongeza ubora wa mbolea hiyo. Vile vile, Serikali itafanya mazungumzo na makampuni ya nje ambayo yako tayari kuwekeza nchini kwa ajili ya kuzalisha mbolea za aina mbalimbali. Lengo ni kuiwezesha nchi yetu katika kipindi kifupi kijacho kujitosheleza kwa mahitaji yake ya ndani ya mbolea na ziada kuuza nje.

 

mgPrint friendly version mg Email this page
Speeches

Hotuba ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, (Mb.), Kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu Na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2008/2009
Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu, katika hafla ya kufunga Kongamano la Utumishi wa Umma tarehe 18 Juni 2008
More Speeches
kk Quotes
Kwenu ninyi Wajasiriamali, Benki imewawezesha. Ni jukumu lenu kuendeleza kile ulicho nacho katika biashara na kupiga hatua. Mmekwishaingia kwenye biashara. Tunategemea msirudi nyuma. Msikubali kufilisika… Mthubutu kufanya maamuzi magumu kibiashara kwani wengi waliofanikiwa katika biashara ni wale waliothubutu. Ni wale waliokubali kukabiliana na changamoto zinazowakabili bila kusitasita.
 
Sherehe za miaka mitano ya Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam,
Machi 15, 2008
More Quotes
Videos
Ufunguzi wa warsha ya Kimataifa ya Taasisi za Maendeleo ya Jamii kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza
11 December 2007
video
video
More Videos
Photo Gallery
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akipongezwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye ikulu ya Chamwino Dodoma.
More Photos
Documents and Publications