Home | News | Waziri Mkuu awaasa vijana wasomi wasikubali kutumiwa hovyo kwenye kampeni
News
Speeches

Hotuba ya Shukrani kwa Wabunge kabla ya Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Kuvunjwa na Mheshimiwa Rais, Ukumbi wa Bunge, Dodoma, 15 Julai 2010...

Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (Mb) Waziri Mkuu Wakati wa Kufungua Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma katika Ukumbi wa African Dreams – Dodoma, tarehe 25 Juni 2010...

More Speeches
Recently Documents

kk Quotes

kama Bunge, lakini mmoja mmoja kama watumishi wa umma, tunao wajibu mkubwa sana wa kuishi na kutenda kwa mfano. Tujiepushe na tamaa zinazoweza kuliingizia Taifa hili hasara kubwa.

Kauli ya Waziri Mkuu kuhitimisha mjadala wa Richmond,
Mkutano wa 18 wa Bunge, Februari 10, 2010
More Quotes
Videos
Photo Gallery

Spika wa Bunge, Samuel Sitta akimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa katika sherehe za kumwapisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenye Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Februari 9, 2008.
More Photos
Documents and Publications


mgPrint friendly version mg Email this page

Waziri Mkuu awaasa vijana wasomi wasikubali kutumiwa hovyo kwenye kampeni

Dodoma,25 June 2010

 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaasa vijana wa vyuo vikuu nchini wasikubali kutumiwa hovyo ili kusababisha uvunjifu wa amani wakati wa kampeni za uchaguzi nchi nzima na badala yake waisadie Serikali kulinda utamaduni na maadili mema ya Watanzania. 
 
“Shirikini katika mchakato mzima kuanzia muda wa kampeni, kura za maoni na hatimaye kupiga kura kwa amani na utulivu. Msikubali kutumiwa katika kusababisha uvunjifu wa amani na vitendo vyovyote nje ya taratibu na kanuni za uchaguzi”, alisema.
 
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Juni 25, 2010) wakati akizungumza na washiriki wa Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma lililofanyika kwenye ukumbi wa African Dreams nje kidogo ya mji wa Dodoma.
 
Pia amewaasa vijana hao wajiepushe na matumizi ya dawa za kulevya, maambukizi ya virusi vya UKIMWI na vurugu za mara kwa mara kwani sicho kilichowapeleka kwenye taasisi hizo.
 
Akifungua kongamano hilo la siku tatu ambalo linashirikisha zaidi ya vijana 800 kutoka vyuo vikuu vinne vya St. John’s, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Mipango na Chuo cha Biashara, Waziri Mkuu amesema vijana ndio kundi kubwa lililoathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya na wao ni mashahidi kwani kila mara wanawaona Vijana wenzao walioathirika kwa kutumia Dawa za Kulevya. 
 
“… Wanaonekana kama wajinga na mara nyingine hupoteza mwelekeo wa maisha kabisa. Wito wangu kwenu kuhusu matumizi ya dawa za kulevya ni kuhakikisha kwamba hamjiingizi katika ulevi huu,” alisisitiza.
 
Akizungumzia kuhusu maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, Waziri Mkuu alisema wanafunzi wa vyuo vikuu ni sehemu ya mkusanyiko mkubwa wa wakazi wa mji wa Dodoma na kwamba hivi sasa wanafikia 20,000 kwa hiyo ni rahisi sana kwao kuwa na mahusiano ya karibu ikiwepo ya kimasomo, kirafiki, na kimapenzi wakati na baada ya masomo.
 
Amewaasa wajilinde wasiambukizwe wala wasiambukize wengine virusi vya UKIMWI na akasisitiza haja ya kupima ili kujua afya zao. “Maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa vijana yamekuwa yakiongezeka siku baada ya siku. Ni jukumu la kila mmoja wenu kukataa kabisa kuwa muathirika wa UKIMWI. Natoa wito kwa watu wote mlioko hapa kuchukua hatua za makusudi za kujilinda ili tusiambukizane au kuambukizwa UKIMWI. Vilevile, kupima ni jambo la msingi ili kujua afya zetu na hivyo kwenda sambamba na Kampeni ya Kitaifa ya Kupima”, alisema.
 
Akisisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana, Waziri Mkuu aliwataka vijana hao watambue wajibu wao mkubwa wanapokuwa vyuoni ambao ni kusoma. “Tumieni muda wenu kuzingatia masomo kwa kujua majukumu yenu ya baadaye. Epukeni kujiingiza katika mambo yasiyokuwa na tija katika masomo na maisha yenu kwa ujumla. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wazazi walezi na wafadhili wenu inahakikisha kwamba ninyi Vijana mnapata elimu bora katika ngazi zote,” alisisitiza.
 
“Taifa hai ni lile lenye watu walioelimika. Lengo la Serikali ni kuona mafanikio yenu katika elimu mnayopata huko vyuoni yanatumika katika kujenga uchumi na kuleta maendeleo. Aidha, hamna budi kuitumia elimu mpatayo katika maisha yenu ya siku kwa siku, kwa kuchanganua mambo kwa umakini na uhakika,” alisisitiza.
 
Akifafanua kuhsu mikopo inayotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu alisema licha ya kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache zinazotoa mikopo kwa wanafunzi, mikopo hiyo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka sambamba na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo.
 
Akitoa mchanganuo wa miaka mitano iliyopita, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2005/2006 wanafunzi 42,729 walipata mikopo ya sh. bilioni 56.1; Mwaka 2006/2007 wanafunzi 47,554 walipata mikopo ya sh. bilioni 76.1; Mwaka 2007/2008 wanafunzi 55,687 walipata mikopo ya sh. bilioni 122.5; Mwaka 2008/2009 wanafunzi 58,798 walipata mikopo ya sh. bilioni 139.7 na Mwaka 2009/2010 wanafunzi 69,560 walipata mikopo ya sh. bilioni 197.3.
 
Ufunguzi wa kongamano hilo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Msekela, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. John’s, Prof. Daimon Mwaga; Makamu Mkuu wa Chuo cha Biashara, Bw. Omary Mohammed Kiputiputi, baadhi ya wabunge na maafisa kutoka Wizara ya Afya.
 
 
 (mwisho)
Help | Disclaimer | Privacy | Site Feedback
Copyrights ©2008-2010, The United Republic of Tanzania, Prime Minister All Rights Reserved
Designed and published by DataVision International (T) Ltd