WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itaangalia mfumo wake wa kodi kuona namna gani ya kujibu kilio cha wawekezaji katika utafutaji wa mafuta na gesi kuwa wanatozwa kodi kwa kuwekeza tu na siyo baada kuzalisha na kuuza bidhaa hizo na kupata faida.
Mhe. Pinda alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuufungua mkutano wa wadau wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es Salaam leo (Jumanne, Juni 01, 2010).
Alisema kuwa Serikali haina budi kuangalia suala hilo kwa vile wawekezaji hao wanayo hoja kuwa badala ya kutozwa kodi wakati wa utafutaji, watozwe baada ya kuzalisha na kupata faida baada ya kuuza bidhaa hizo.
Ilielezwa kwamba nchini Tanzania, wawekezaji katika utafutaji wa mafuta na gesi, hutozwa kodi ya asilimia 15, wakati Kenya hutozwa asilimia 4.5 na nchi nyingine hawatozwi kabisa mpaka wapate mafuta na gesi na kuzalisha na kuuza.
Mapema katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Mkuu, hata hivyo, aliwataka wawekezaji katika sekta hiyo kuwa na miradi ya kusaidia kijamii katika maeneo wanakofanyia shughuli zao.
Mhe. Pinda pia aliyataka makampuni ya wawekezaji nchini kutumia bidhaa na huduma za Kitanzania madhali vitu hivyo vinapatikana nchini kwa viwango bora na kwa wingi unaohitajika, kuendeleza jitihada za serikali za kutoa ajira na kuwawezesha wananchi.
Akimkaribisha Mhe. Pinda kufungua mkutano huo, Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja alisema wadau wa uwekezaji katika sekta ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ni muhimu kukutana kubadilishana mawazo.
Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha Wawekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi (Oil and Gas Association of Tanzania – OGAT) na umewashirikisha wawakilishi kutoka Serikalini na chama hicho.
Utafutaji wa gesi na mafuta, umekuwa ukiendelea nchini tangu miaka ya 1950 na ingawa mafuta hayajagunduliwa, gesi imepatikana na imeanza kutumika nchini tangu mwaka 2004 kwa ajili ya kuzalisha kiasi cha umeme na kuendesha baadhi ya viwanda.
Mikoa ya Lindi na Mtwara inapata umeme unaotengenezwa kwa nguvu za gesi na viwanda vipatavyo 25 jijini Dar es Salaam mitambo yake huzalisha kwa kutumia nguvu za gesi.