|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kufanyika kwa Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia kuhusu Bara la Afrika (World Economic Forum on Africa-WEF) hapa nchini ni fursa muafaka ya kuinadi Tanzania na kuangalia jinsi gani nchi inaweza kunufaika na fursa hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Mei 02, 2010) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambako mkutano huo utafanyika.
“Kwetu ni fursa ya kuangalia jinsi ya kukuza uchumi kwa maana ya kilimo, mifugo na uvuvi lakini pia ni nafasi ya kuangalia Afrika kama Bara kuna fursa zipi za uwekezaji na kuna vikwazo vipi katika uwekezaji; na ni kwa namna gani tunaweza kulisadia bara la Afrika kukuza uchumi wake,” alisema.
Alisema kufanyika kwa mkutano huo pia kunatoa fursa kwa wajumbe watakaoshiriki kwenye mkutano huo waone ni kitu gani wanaweza kufanya hapa nchini pindi wakirudi makwao.
Kabla ya kukagua ukumbi huo, Waziri Mkuu alitembezwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) ambako wajumbe wa mkutano wataanza kuwasili kuanzia leo.
Akiwa huko alikagua ukumbi wa kupokelea wageni mashuhuri (VIPs) wanaowasili na kuondoka nchini ambao alikuta uko katika hatua za mwisho za ujenzi. Pia alikagua maandalizi katika eneo la wageni wa kawaida wanaowasili nchini hasa idara za afya, uhamiaji na forodha.
Akizungumzia maandalizi aliyoyakuta, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na kazi iliyofanywa kwa ajili ya mkutano huo unaotarajiwa kuanza Jumatano ijayo. “Tumekuwa na maandalizi ya muda mrefu, lakini kama Serikali ilibidi tufike kuona hali halisi na kujiridhisha na jinsi kazi inavyokwenda… mambo yanakwenda vizuri, kuna madogo madogo yamebaki na nimewaeleza Kamati,” alisema Waziri Mkuu.
Naye Mkurugenzi wa WEF na Mkuu wa Kanda ya Afrika, Bi. Katherine Tweedie alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanatarajia kupokea wageni zaidi ya 1,000 kutoka nchi 85 duniani wakiwemo Wakuu wa Nchi na Wawakilishi wa Serikali 12.
Alisema tangu taasisi hiyo ianze kuandaa mikutano ya aina hii, haijawahi kupata washiriki wengi kama ilivyo katika mkutano huu unaotarajiwa kuanza Jumatano, Mei 5 – 7, 2010. Alimshukuru Waziri Mkuu kwa utayari ulioonyeshwa na Serikali ya Tanzania katika kipindi chote cha maandalizi na ushirikiano wa hali ya juu iliopata kutoka kwa wahusika.
Bi. Tweedie alisema leo jioni (Mei 2, 2010) kundi la vijana 280 wanatarajia kuwasili nchini kwa ajili ya Mkutano wao wa Viongozi Wachanga wa Dunia (Young Global Leaders - YGL) ambao mbali ya kuhudhuria mkutano wao hadi Mei 7, 2010; pia watashiriki huduma za jamii katika maeneo mbalimbali ya jijini ambako wamepangiwa kutembelea.
Hii ni mara ya kwanza mkutano wa WEF kufanyika eneo la Afrika Mashariki. Mara ya mwisho mkutano kama huo ulifanyika mjini Cape Town, nchini Afrika ya Kusini mwaka 2008.
Mapema, akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, alisema maandalizi ni mazuri na kwamba kuna mabasi madogo zaidi ya 50 ambayo yameandaliwa kwa ajili ya kupokea wageni na kuwafikisha katika hoteli walizopanga.
Alisema wanataraji kuwa ifikapo kesho jioni mambo yote yatakuwa yamekamilika kwa maana ya kumbi na jengo la viongozi mashuhuri.
Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Rethinking Africa’s Growth Strategy” (Kufikiria Upya Mkakati wa Kukua kwa Uchumi wa Afrika) ambapo Mada za Mkutano huo zitazungumzia pamoja na mambo mengine; Elimu ya Juu kwa Bara la Afrika, Hali ya Maliasili hadi 2030; Tanzania kama Sehemu ya Kipekee ya Uwekezaji; Tanzania ya Kesho; Kuiwezesha Afrika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mada nyingine ni MDG 3: Kuwawezesha Wanawake wa Afrika; Uwezo wa Kuzalisha Bidhaa Nchini na Kuuza kwenye Masoko ya Nje; Kuimarisha Utawala wa Sheria; Uhusiano wa Maji, Chakula na Nishati katika Maendeleo; Mapambano Dhidi ya Rushwa; Mbinu za Kuchochea Kukua kwa Biashara; Jinsi ya Kuziba Pengo la Nishati; Mtazamo Mpya wa Kilimo Barani Afrika; Kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; Kukua Kwa Miundombinu; Ushirikiano wa Nchi za Afrika katika Maendeleo ya Kiuchumi.
(mwisho) |