|
TANZANIA na Msumbiji zimekubaliana kuendeleza biashara baina ya nchi hizo jirani kwa kusisitiza kuwa Sekta Binafsi ihusishwe zaidi.
Hayo yamo katika Taarifa ya Pamoja mwishoni mwa ziara ya siku tatu ya Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mhe. Aires Bonifacio Baptista Ali, nchini Tanzania, kwa mwaliko wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Taarifa hiyo, iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jijini Dar es Salaam leo asubuhi (Jumapili, Machi 7, 2010) ilisema Mawaziri Wakuu hao walisisitiza haja ya kuimarishwa kwa nguvu zote biashara baina ya nchi zao.
“Kwa maana hiyo, walisisitiza umuhimu wa kuihusisha zaidi Sekta Binafsi katika jambo hilo na wadau wote watimize wajibu wao wa kuhakikisha uhusiano wa kibiashara unaimarishwa,” taarifa ilisema.
Ilisema kuwa Mawaziri Wakuu hao walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta kama vile Kilimo, Madini, Elimu, Mafunzo, Afya, Uvuvi, Serikali za Mitaa, Biashara, Uwekezaji na Utalii.
Walieleza matumaini yao kuwa mkutano ujao wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano utaziwezesha nchi hizo mbili kufanya mapitio ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika vikao vilivyotangulia na kupanga mikakati ya kutimizwa kwa malengo yaliyodhamiriwa.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Mawaziri Wakuu hao wawili walieleza kuridhishwa kwao na kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Umoja linalounganisha nchi hizo mbili kwa barabara mbili kuvuka Mto Ruvuma na kusema kuwa kuanza kutumika kwa Daraja hilo kutafungua milango mipya ya ushirikiano baina ya wananchi wa nchi hizi mbili kutokana na kuongezeka kwa uchukuzi kwa njia ya barabara, kuongezeka kwa biashara, utalii, uwekezaji na mahusiano baina ya watu.
“Walisisitiza haja ya kuhakikisha kuwa miundiombinu ya huduma muhimu na za msingi kwenye mipaka ya nchi hizo mbili Darajani inaanza kazi mara tu Daraja hilo litakapozinduliwa rasmi”.
Waziri Mkuu wa Msumbiji, akiwa na ujumbe mzito, aliwasili Dar e Salaam Ijumaa usiku (Machi 5, 2010) na kulakiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu Pinda pamoja na Mawaziri wengine na Maofisa waandamizi wa Chama na Serikali.
Katika ujumbe wa Waziri Mkuu Ali walikuwemo pia Waziri wa Ujenzi na Nyumba, Mhe. Cadmiel Muthemba; Waziri wa Utamaduni, Mhe. Armando Artur Joao; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Dk. Eduardo Koloma; Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Pedro Couto na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama kinachotawala cha FRELIMO, Mhe. Jenerali (Mstaafu) Raimundo Pachinuapa.
Mawaziri Wakuu hao wawili walikuwa na mazungumzo rasmi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Jumamosi (Machi 6, 2010) asubuhi ambapo walifanya mapitio na kujadili masuala kadhaa ya uhusiano wa nchi hizi mbili. Baadaye Waziri Mkuu Ali aliitembelea Zanzibar.
Waziri Mkuu huyo wa Msumbiji pia alimtembelea Rais Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam kwenda kumsalimia.
Jana usiku (Jumamosi, Machi 6, 2010), Waziri Mkuu Pia alimuandalia mgeni wake chakula rasmi cha usiku na katika hotuba zao Mawaziri Wakuu hao walisisitiza tena haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo baina ya nchi hizi mbili.
Waziri Mkuu Ali, ambaye alitoa mwaliko kwa Waziri Mkuu Pinda kutembelea Msumbiji katika tarehe itakayokubaliwa baadaye, leo asubuhi (Jumapili Machi 7, 2010) alipanda ndege kurejea Maputo.
(mwisho)
|