|
*Asema Ofisi za DED, DC wa Uyui zihame mjini Tabora
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mikoa yote nchini imeunganishwa kwa barabara kuu ifikapo mwaka 2016 ili zipitike kwa nyakati zote za mwaka.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Februari 23, 2010) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wakazi wa Kata za Ibushi na Kigwa wilayani Uyui, Tabora katika siku ya nne ya ziara yake mkoani hapa.
Akiwa Ibushi, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya ujenzi wa ofisi za Halmashauri hiyo kuanza mara moja ili kuleta maendeleo ya haraka katika wilaya hiyo ambayo ilipata hadhi ya kuwa wilaya Julai 28, 2002.
“Ofisi za Halmashauri na Mkuu wa Wilaya zihame mjini zije Isikizya ndipo maendeleo yatakuja haraka... kwa sababu mtu hawezi kuishi mjini kwenye umeme na lami halafu aamke asubuhi kuja kufanya kazi huku kila siku na kuwaleeteni maendeleo,” alisema.
Alisema kama viongozi watahamia kule huduma za muhimu kama posta, hospitali ya wilaya, huduma za TANESCO na nyumba za kuishi watumishi zitapatikana haraka. Isikizya ni eneo lililotengwa kwa ajili ya kujenga makao makuu ya wilaya ya Uyui ambalo liko km. 40 kutoka Tabora mjini.
Akijibu swali la Bw. Juma Mohamed Kalindimya, mkazi wa Ibushi ambaye alitaka kujua ni lini serikali itaweka lami kwenye barabra ya kutoka Nzega hadi Tabora, Waziri Mkuu alisema Serikali imejipanga kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara kuu nchini ifikapo mwaka 2012 na awamu ya pili itakamilika ifikapo mwaka 2016.
“Taratibu za kuiwezesha barabara hii ili iwe na kiwango cha lami zimekwishakamilika, naamini itaanza kujengwa kabla ya bajeti ya mwaka ujao kuanza... hii siyo barabara pekee ambayo imebaki, zipo za Tabora – Mpanda, Tabora – Ipole - Mbeya, na Kigoma hadi Mpanda,” alisema.
Akiwa katika kata ya Kigwa “B” kwenye jimbo la Igalula ambako alikwenda kuzindua Kituo cha Habari kwa Wakulima (Ward Agricultural Resource Centre - WARC), Waziri Mkuu aliwataka wakazi wa kata hiyo wakitumie vizuri kituo chao ili kupata taarifa ambazo zitawasadia kuboresha kilimo chao.
Mmoja wa wakazi waliouliza maswali kwa Waziri Mkuu, Bw. Sadala Juma Sadala ambaye ni mkazi wa Kigwa, alitaka kujua ni lini Serikali itawajengea barabara ya kutoka Tabora hadi Itigi kwani asilimia 90 ya wakazi wa jimbo la Igalula wanategemea usafiri wa reli na barabara.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema barabara hiyo imegawanywa katika awamu tatu ambazo ni Tabora – Nyahua katika awamu ya kwanza, Nyahua – Chaya katika awamu ya pili na Chaya – Itigi – Manyoni katika awamu ya tatu ambazo mkataba wake utasainiwa kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Waziri Mkuu ambaye amefuatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige, leo (Jumatano, Februari 24, 2010), atakuwa Manispaa ya Tabora ambako atakagua kituo cha mifugo, josho na bwawa; atazindua sekondari ya Nkumba na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa majengo katika shule ya sekondari ya wasichana ya Tabora ambao unafadhiliwa na UNHCR. Jioni ataelekea wilaya ya Urambo.
(mwisho)
|