|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema ni lazima Chama cha Mapinduzi (CCM) kiwakatae watu wanaotumia fedha kutafuta nafasi za uongozi kwani viongozi wa aina hiyo wakipita Serikali itajikuta ina viongozi wasiofaa ila wako pale kwa sababu tu wana pesa.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Februari 6, 2010) wakati akiwahutubia wakazi wa wilaya ya Mpwapwa kwenye maadhimisho ya miaka 33 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kimkoa wilayani humo, mkoani Dodoma.
Alisema CCM iliangalia utaratibu unaotumika katika kupitisha viongozi na kubaini kuwa kuna kasoro ndipo ikafikia uamuzi wa kubadili mfumo huo ili wanaogombea ubunge na udiwani waende kupigiwa kura kuanzia katika ngazi ya tawi.
Alisema uamuzi huo mpya unatoa nafasi kwa wananchi kuamua kama mgombea anawafaa au hawafai na kwamba endapo watabaini kuna watu ambao wanakuja kwa staili ya ‘mkao wa kula’ waamue kusema hapana mara moja.
“Kama kuna mtu anakuja na staili ya mkao wa kula ni lazima wote tuseme hapana, la sivyo tutakuwa na viongozi wasiofaa na wako madarakani eti kwa sababu tu wana pesa na walitumia pesa zao kuhonga wananchi,” alisisitiza.
“Ni lazima Chama kikatae kuwapitisha watu wa aina hii... muanze kuwachuja tangu wilayani na wala hakuna haja ya kuwaleta kwenye Kamati Kuu... haiwezekani kuwa na viongozi ambao wanawanunua kwa sh. 5,000/- au sh. 20,000/-,” alisema.
“Kama Chama ni lazima tuendelee kukataa wenye tamaa ya mali kupindukia kwa sababu matokeo yake ni kujikuta tuna watu wenye kula rushwa... huwa najiuliza sababu za watu kujilimbikizia mali kupita kiasi wakati mwisho wetu wote ni kichumba cha pembe nne,” alisema.
Alisema Watanzania wasikubali kuwa na viongozi wenye kupenda kujilimbikizia mali kwa sababu mwisho wa yote watatumia nafasi hizo kuhonga ili kupata tenda na mikataba mikubwa. “Haiwezekani kiongozi upende kujilimbikizia mali ili upate umaarufu tu, ni lazima utatumia utajiri huo kuhonga ili kupata kandarasi na mikataba mikubwa,” alisema huku akisahngiliwa na wakazi hao.
Alionya kwamba ili kutibu ugonjwa huo wa kuwa na viongozi wenye kupenda mali, vyama vya siasa havina budi kurudi kwenye chaguzi za vyama vyao. “Lazima turudi kwenye vyama vyetu ili kutibu ugonjwa huu, mkiwa na viongozi wachafu siyo rahisi kuundaSerikali iliyo safi.”
Alisema japokuwa suala la rushwa ni la mtu mmoja mmoja, lakini kila chama hakina budi kusema kinachukua hatua gani dhidi ya huyo mtu mmoja mmoja ili kuepusha tabia hii miongoni mwa wagombea nafasi za uongozi.
(mwisho)
|