|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameitaka Taasisi ya Watunga Sera kuhusu Hifadhi za Jamii Afrika Mashariki na Kati (ECASSA), izisaidie Serikali za nchi husika kutafuta njia rahisi zitakazoondoa kasoro zilizopo kwenye mafao ya wafanyakazi hasa wakati huu ambao nchi za Afrika Mashariki zipo kwenye mchakato wa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Waziri Mkuu Pinda alitoa wito huo leo asubuhi (Ijumaa, Januari 29, 2010) wakati akifungua mkutano wa pili wa nchi nane ambazo ni wanachama wa ECASSA. Mkutano huo wa siku tatu ulianza jana (Alhamisi, Januari 28, 2010) katika ukumbi wa hoteli ya Nyumbani jijini Mwanza.
Waziri Mkuu alisema kwamba Serikali ya Tanzania inathamini na kutambua kazi nzuri zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha na kutoa mafao miongoni mwa wanachama wake.
“…ECASSA inahitajika kutoa misaada zaidi kwa wanachama wa mifuko hii ili kuongeza mapato na michango yao kwa ajili ya kukuza uchumi wao; hali kadhalika kwa maendeleo ya nchi zao,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alitoa mfano kwamba bila msaada wa watunga sera, itakuwa ni vigumu kwa wafanyakazi wa nchi za Afrika Mashariki kufaidika na soko la pamoja kwa vile kunaweza kuibuka migongano inayohusiana na mafao kati ya wafanyakazi wa nchi moja na nchi nyingine.
Alisema kwamba bila kufanya hivyo wafanyakazi wengi watajikuta wakipoteza haki zao za kutaka mafao yao. “Kwa kweli watunga sera watusaidie sana katika kuainisha na hata kutunga sera nzuri zitakazoondoa migongano, vinginevyo watumishi wengi watapoteza mafao yao wakati tukianza soko la pamoja la Afrika Mashariki,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili mifuko ya jamii katika nchi za Afrika Mashariki kuwa ni pamoja na kuwepo kwa tofauti kati ya sera za uchumi na sera za mifuko ya jamii pamoja na tofauti katika uchumi kati ya eneo moja na eneo jingine.
Waziri Mkuu aliwataka watunga sera kushirikiana na Serikali zao kuhakikisha kwamba mifuko ya Jamii inawanufaisha wanachama pamoja na wategemezi wao.
Mapema, Mwenyekiti wa ECASSA, Bw. Abdulwakil Hafidh alisema kuwa mada kuu katika mkutano huo ni Utawala katika Hifadhi ya Jamii ambapo zaidi ya washiriki 70 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Sudani, Rwanda, Zambia, Burundi, Mauritus na Tanzania wamehudhuria.
Alisema kwamba mkutano wa kwanza wa ECASSA ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwaka 2000.
mwisho
|