|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itamsomesha mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi Pendo Michael (13) ambaye alifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana katika Shule ya Msingi Maalumu ya Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na kushindwa kuendelea na shule kwa sababu ya kukosa fedha.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Januari 29, 2010) kwenye ziara ya kushtukiza aliyoifanya shuleni hapo ambapo alipewa taarifa za mwanafunzi huyo na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Juma Abdallah ya kuwa tangu achaguliwe kujiunga na masomo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora ameshindwa kufanya hivyo kutokana na kukosa fedha.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Pendo alitelekezwa na wazazi wake mara baada ya kuletwa shuleni hapa tangu mwaka 2008… amefaulu kuendelea na masomo ya sekondari lakini ameshindwa kwenda shule kutokana na kukosa fedha,” alisema Mwalimu Abdallah.
Alisema: “Wazazi na walezi wanapowafikisha watoto wenye ulemavu wa ngozi kituoni kwetu hapa huwa hawarudi kuja kuwaona, matokeo yake shule ndiyo inabeba mzigo wa kuwatunza kwa maana ya malezi ya kawaida na ya kufundisha. Tangu Pendo afanye mtihani na matokeo yake kutangazwa, wazazi wake wanaoishi Geita hawajaja kumuona, hili ni tatizo kubwa hapa shuleni kwetu ….”
Baada ya kupewa taarifa hizo, Waziri Mkuu alisema Serikali imesikia kilio cha walimu wa shule ya Mitindo juu ya matatizo yanayoikabili shule hiyo yakiwemo matatizo ya maji na vifaa vya kufundishia na kuahidi kwamba yatapatiwa ufumbuzi mara moja.
“Lakini hili la Pendo, tutamsomesha maana hakuna sababu ya kutofanya hivyo, kafaulu mtihani wake, sisi serikalini tutachukua jukumu la kumsomesha na niahidi kuwa tutampeleka Tabora ili aendelee na masomo yake,” alisema.
Shule ya Msingi Maalum ya Mitindo ina zaidi ya wanafunzi zaidi ya 1,000 wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi; wasioona na wenye uono hafifu; wenye ulemavu wa viungo na wasio na ulemavu kabisa.
(mwisho) |