|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda leo (Jumatatu, Januari 18, 2010) amepokea viti 10 vya watu wenye ulemavu vyenye thamani ya sh. milioni 1.5/- kutoka kwa Klabu ya Lions ya Dar es Salaam City.
Akipokea viti hivyo ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema anaishukuru sana taasisi hiyo kwa msaada huo na kuahidi kuwa viti hivyo vitapelekwa mikoa ya Kigoma, Mbeya, Rukwa, Ruvuma na Iringa ambako hakuna matawi ya klabu hiyo.
Pia alisema taasisi zinazotoa misaada kwa jamii zinakabiliwa na changamoto ya kusema kuwa misaada waliyotoa imetosha na kuwaomba waziangalie zaidi taasisi zinazohudumia watu wenye mtindio wa ubongo na kwenye hospitali.
“Taasisi zinazotoa misaada zinakabiliwa na changamoto ya kutokusema misaada mliyotoa imetosha kwa sababu watu wenye uhitaji wanaibuka kila siku… wenye shida ni wengi na ninyi ndiyo wa kuwasaidia,” alisema.
Mapema akikabidhi viti hivyo, Gavana wa Lions katika wilaya 411B, Bw. Abdul Majid Khan alisema tangu mwaka 2008 wamekwishatoa jumla ya viti 500 na kumwahidi Waziri Mkuu kwamba wana mpango wa kufungua matawi kwenye mikoa ya Iringa na Mbeya ili mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iweze uwakilishi kwenye klabu hiyo.
Akizungumzia huduma ambazo klabu hiyo imekwishatoa, alisema katika miaka 35 ambayo klabu hiyo imekuwa ikitoa huduma, wamekwishachimba visima 50 vya maji safi na wametoa huduma kwa wagonjwa wa macho 7,000 na kwamba wakibainika na mtoto wa jicho hupewa huduma ya upasuaji wa macho.
“Pia tunasaidia kupeleka India watoto wenye matatizo ya moyo ili wapate matibabu zaidi na tunasaidia ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali hapa nchini,” alisema.
Alisema klabu hiyo ina matawi saba jijini Dar es Salaam, matawi manne jijini Arusha na matawi matano jijini Mwanza. Mengine ni Kilimanjaro (manne), Shinyanga, Bunda na Morogoro ambako kuna tawi moja moja.
(mwisho) |