|
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amerejea Dar es Salaam leo mchana (Alhamisi, Oktoba 8, 2009) kutoka Geneva ambako alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (International Telecommunication Union – ITU).
Akiwa Geneva, Waziri Mkuu alishiriki katika ufunguzi wa mkutano huo (Jumatatu, Oktoba 5, 2009) na kuhutubia kikao cha pamoja cha wakuu wa nchi na maofisa watendaji wakuu wa mashirika na makampuni ya teknolojia ya habari na mawasiliano duniani.
Katika kikao hicho cha pamoja, Mhe. Pinda alishauri kufikiria utoaji wa elimu duniani kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ili kupunguza matumizi ya vitabu vya kawaida na machapisho mengine.
Alisema matumizi kwa wingi ya vitabu na machapisho mengine yanahitaji karatasi zinazosababisha uharibifu mkubwa wa misitu na kuleta mabadiliko ya hali ya hewa yanayoiathiri dunia hivi sasa.
Kwenye mkutano huo Waziri Mkuu Pinda alifuatana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Peter Msolla na Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Haji Machano.
Mhe. Pinda pia alitembelea mabanda ya maonyesho ya mashirika na makampuni mbalimbali ya teknolojia ya habari na mawasiliano, likiwemo banda la Tanzania la Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA).
(mwisho) |