Logo
Tuesday, 14 October 2014 10:45    PDF 

 

TAMKO LA WAZIRI MKUU KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA UPUNGUZAJI WA ATHARI ZA MAAFA DUNIANI TAREHE 13 OKTOBA, 2014

Ndugu Wananchi,

Tarehe 13 Oktoba, 2014 ni Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa Duniani (International Day for Disaster Reduction). Siku hii huadhimishwa tarehe 13 Oktoba ya kila mwaka. Kama ilivyo kwa miaka yote tangu siku hiyo ilipoanzishwa katika miaka ya 1990. Sekretarieti ya Upunguzaji wa Athari za Maafa ya Umoja wa Mataifa hutoa Kaulimbiu ya mwaka husika. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema, Uthabiti Daima – MITAZAMO JUU YA WAZEE KATIKA MAENEO YANAYOWEZA KUKUMBWA NA MAAFA” (Resilience is for life – PERCEPTIONS ON OLDER PERSONS IN POTENTIAL DISASTER AREAS).

Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa kwa mwaka huu imewalenga wazee. Lengo hasa ikiwa, kuangalia uhitaji walionao wakati wa maafa na athari zake, kutambua nafasi na michango ya wazee katika maafa kulingana na uzoefu walionao kutokana na wingi wa miaka waliyoishi, Waswahili wanasema “kuishi kwingi kuona mengi”.  Dunia imekuwa ikikumbwa na mabadiliko makubwa yenye athari nyingi kwa wakazi wake na mengine kuchochea na ongezeko la uwezekano wa maafa ikiwemo; mabadiliko ya tabia nchi, milipuko ya magonjwa, masuala ya ugaidi, kukua kwa teknolojia na ongezeko la matukio ya mauaji.

Wazee ni kundi ambalo limeonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika. Hali hii imechangiwa zaidi na nafasi ndogo wanayopata wazee katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Katika baadhi ya nchi za Afrika zipo imani mbalimbali potofu juu ya wazee, hii hupunguza uthamani wao ndani ya jamii hata ushiriki katika mambo ya maendeleo. Hivyo, maafa yanapotokea wazee wapo katika nafasi ya kuathirika zaidi kwani inaaminika kuwa hupoteza nguvu nyingi hivyo kuhitaji misaada ya ziada na haraka.

Ndugu Wananchi, leo hii idadi ya watu duniani ni zaidi bilioni 7 ambao ni ongezeko kubwa kulinganisha miaka ya nyuma. Idadi ya wazee inazidi kuongezeka duniani, takriban watu milioni 700 au asilimia 10 ya idadi ya watu duniani wana umri juu miaka 60, na ifikapo mwaka 2030, kutakuwa na watu wengi wenye umri zaidi ya miaka 60 kuliko watu wenye umri chini ya miaka 10. Inasemekana kufikia 2050 itakuwa mara mbili ambayo ni sawa na watu bilioni mbili.

Katika nchi yetu ya Tanzania, takwimu zinaonesha wazee wapo 2,507,568 hii ikiwa ni asilimia 5.6 ya Wananchi wote. Tofauti na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 ambapo idadi ya wazee ilikuwa ni asilimia 4.0, takwimu hizi zinaonesha idadi ya wazee imeongezeka kwa kiwango cha asilimia 1.6. Ongezeko linaashiria kuboreka kwa huduma za kijamii ikiwemo: afya, maji safi na salama, chakula, elimu na mazingira bora. Wakati hali hii ikiashiria ushindi katika maendeleo, kwa upande mwingine, ongezeko la hali ya juu la mabadiliko ya  hali ya hewa na matukio ya maafa kunasababisha kuongezeka kwa uwezekano wa wazee kuathirika na maafa, hii inatokana na uwezo mdogo wa kutekeleza shughuli za upunguzaji wa athari za maafa kwa kizazi cha wazee. Pamoja na changamoto ya kuwa na uwezo mdogo, bado watu wenye mahitaji maalum hawajapewa kipaumbele stahiki katika upunguzaji wa athati za maafa.

Ndugu Wananchi, Maslahi ya wazee pia yamezungumzwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo inatamka wazi kuwa wazee kupewa hashima na kupata hifadhi kutoka serikalini na kwa jamii kwa ujumla. Vilevile, katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa suala la Haki za Wazee limetamkwa na kuainishwa. Pia katika Sera yaTaifa ya Wazee (2003), Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2003 na Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2001 maslahi ya Wazee yamezungumzwa kwa kina.Vilevile Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 inatambua umuhimu wa wazee na watu wenye mahitaji maalumu kupewa kipaumbele katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya menejimenti ya maafa.

Pamoja na matamko haya, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuboresha maslahi ya kundi hili muhimu na lenye hazina kubwa, bado Serikali na wadau wengine wa maendeleo wanapaswa kuongeza juhudi kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee. Natoa wito kwa watendaji wote wa Serikali na wadau wengine wanaohusika katika kutoa huduma kwa Wazee kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu.

Itakumbukwa kuwa, tangu mwaka 2002 Nchi yetu ilipoungana na Nchi nyingine duniani kutia saini Mkataba wa Kimataifa wa Wazee ilikuwa ni kielelezo tosha cha nia njema ya kuendelea kuboresha na kuendelea kubuni na kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha ya Wazee. Serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali na kutoa huduma kwa wazee katika makazi 17 ya wazee yanayoendeshwa na Serikali.   Kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010 jumla ya wazee 6,512 walihudumiwa. Kwa mwaka 2013/2014 jumla ya wazee 1,226 walipatiwa huduma muhimu za kujikimu; kama chakula, afya na malazi. Vilevile Serikali imekuwa ikiratibu shughuli za utoaji wa huduma kwa wazee katika makazi 24 yanayosimamiwa na Mashirika ya dini. Ili kuhakikisha Wazee wanapata huduma za afya kwa urahisi, Serikali imeanzisha utaratibu wa kila hospitali na vituo vya afya kuwa na kliniki maalum kwa ajili ya wazee na kuelekeza wapatiwe huduma za afya bure.

Katika Kutekeleza Sera yaTaifa ya Wazee (2003) na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9,ya mwaka 2010, Serikali kwa kushirikiana na  mashirika ya hiari inatekeleza mradi wa kuwatenganisha Watu wenye Ulemavu na Wazee wanaotunzwa katika makazi kwa lengo la kujenga jamii jumuishi inayojali haki na ustawi wa makundi maalum katika jamii. Aidha kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati; lakini kwa kushirikiana na wadau, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba huduma zinatolewa kwa wazee.

Ndugu Wananchi, Ni dhahiri kwamba wazee wanaonekana kusahaulika na kutotambuliwa na kupewa nafasi na  ushiriki wao katika kukabili athari za maafa. Wazee ni watu wenye hazina kubwa ndani yao ikiwemo uwezo mkubwa wa kujitolea, kujali, wenye huruma, kushauri, kuongoza na kushiriki katika mambo yanayo ihusu jamii.  Katika maadhimisho ya mwaka huu ni vyema kujikita katika mambo muhimu yanayohusu wazee na maafa kama ifuatavyo:-

i. Uhitaji: Wazee wana mahitaji maalum ambayo lazima yaeleweke na yafanyiwe kazi katika shughuli za upunguzaji wa athari za maafa.

ii. Kutotambulika: uwezekano wa kuathirika na uwezo wa kukabili maafa wa Wazee mara nyingi hautiliwi maanani. Ukusanyaji wa takwimu juu ya umri na jinsia ni muhimu ili kuhakikisha wazee na watu wengine walio katika hatari kubwa ya kuathirika wanajulikana na kuungwa mkono katika upunguzaji wa athari za maafa.

iii. Thamani kubwa: Wazee wana maarifa ya miaka mingi, ujuzi na hekima waliyonayo ni hazina yenye thamani kubwa katika kupunguza athari za maafa, hivyo ni lazima watambuliwe na kushirikishwa katika upunguzaji wa athari za maafa.

Ili kuhakikisha wazee wanashiriki kikamilifu katika shughuli za upunguzaji wa athari za maafa, hatuna budi kutafakari yafuatayo:-

· Nafasi ya wazee katika Maafa

· Kujadili michango ya wazee  Kabla na Baada ya maafa kutokea

· Kuhamasisha umuhimu wa kuwajali na kuwatunza wazee ili wapate sehemu salama ya kukimbilia

· Jamii na Serikali kuweka mazingira rafiki ya kuwasaidia wazee ili kupunguza athari za maafa.

Ndugu Wananchi, yapo mambo ya msingi ambayo Serikali imeyawekea mkazo na kuyafanyia utekelezaji ikiwa ni namna ya kufikia lengo la kuelimisha jamii juu ya nafasi ya wazee katika maeneo yenye uwezekano wa kukumbwa na athari za maafa. Ikumbukwe kwamba ushiriki wa wazee katika masuala ya jamii na michango yao katika maafa yanaweza kuwa upande wa kutoa ushauri ikiwa ni watu wanaoheshimika na wenye mawazo chanya kulingana na uzoefu wao, hekima na busara walizonazo juu ya mambo yanayohusu maafa.

Ni wazi kuwa Serikali imejitahidi kuhakikisha wazee wanaandaliwa mazingira rafiki ili kukabiliana na athari za maafa ikiwemo kuwepo kwa vituo vya afya vinavyowahudumia wazee, vituo vya kutunza wazee kama kituo cha Bukumbi kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza pamoja na Kambi ya kulea wazee na wasiojiweza ya Funga Funga mkoani Morogoro, upatikanaji wa maji safi na salama karibu na maeneo wanayoishi, ulinzi na usalama pamoja na uboreshwaji wa huduma zabarabara.

Hivyo ninatoa wito kwa Jamii, Mashirika ya Umma, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha wazee wapo katika mazingira salama ya kulindwa, kutunzwa, kuhudumiwa na kusaidiwa katika kujikinga na maafa na athari zake. Kwa kuzingatia hayo, tutakuwa tumefanikisha Uthabiti Daima na kujenga mwamko kwa jamii kuhusu athari  za Maafa kwa wazee na kila mmoja wetu kuchukua hatua stahiki za kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea tukitambua kuwa maafa hutokea wakati wote, ni jukumu la kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kupunguza athari za Maafa.

 

--Mwisho--

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday50
mod_vvisit_counterYesterday107
mod_vvisit_counterThis week50
mod_vvisit_counterLast week753
mod_vvisit_counterThis month2960
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days525145
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved