Logo
Friday, 09 February 2018 00:00    PDF 

 

Hotuba ya Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuahirisha Mkutano wa Kumi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 9 Februari, 2018

UTANGULIZI

Shukrani

1. Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa fadhila na rehema kwa kutujaalia afya njema hadi leo hii tunapohitimisha Mkutano wa Kumi wa Bunge lako Tukufu ambao umetuweka mjini Dodoma kwa takriban wiki mbili. Kwa kuwa huu ni mkutano wa kwanza tangu mwaka huu uanze, ninakutakia wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge na watumishi wote wa Bunge Heri ya Mwaka Mpya 2018.

Salamu za Pole

2. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa naungana tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu za pole kwa Wananchi wa Jimbo la Songea Mjini, kwa Bunge lako Tukufu na kwa familia ya marehemu Leonidas Gama, aliyetangulia mbele za haki wakati akiendelea kulitumikia Taifa. Vilevile, natoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na familia ya marehemu Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyewahi kulitumikia Bunge hili, Serikali na ni miongoni mwa waasisi wa Chama cha Mapinduzi. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahala pema peponi. Amina!

3. Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Desemba, 2017 Taifa letu lilikumbwa na msiba mzito baada ya kuondokewa na askari wetu 14, ambao tutaendelea kuwakumbuka kwa ushupavu na ushujaa wao wakati wakitekeleza majukumu yao ya Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuuawa na waasi katika shambulio la kushtukiza. Kwa majonzi makubwa kabisa naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huo mkubwa.

4. Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, natumia fursa hii kutoa salamu za pole kwa Mhe. Kangi Lugola (Mb.), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kufiwa na mwenza wake. Vilevile, natoa salamu za pole kwa familia na watumishi wa mahakama kwa kifo cha Jaji Mstaafu, Mhe. Robert Kisanga ambaye atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kulitumikia Taifa letu katika nyadhifa mbalimbali. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahala pema peponi. Amina!

5. Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata ulemavu katika matukio mbalimbali ikiwemo ajali za vyombo vya usafiri. Pia, wale wote waliokumbwa na janga la mafuriko yaliyosababisha uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo miundombinu na hata vifo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu yakiwemo Chemba (Dodoma), Dar es Salaam na Kilosa (Morogoro).

Pongezi

6. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika mkutano huu wa Kumi wa Bunge lako tukufu, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walionitangulia kumpongeza Mhe. Dotto Mashaka Biteko (Mbunge wa Jimbo la Bukombe) kwa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri wa Madini. Napenda pia kuwapongeza Wabunge waliochaguliwa, Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Jimbo la Songea Mjini), Mhe. Justin Joseph Monko (Jimbo la Singida Kaskazini) na Mhe. Dkt. Stephen Lemomo Kisurwa (Jimbo la Longido).

7. Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Adelardus Kilangi, kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ni matumaini yangu kwamba uzoefu na umahiri wake katika masuala ya sheria, utasaidia sana katika kuishauri Serikali na Bunge. Aidha, nampongeza Mheshimiwa George Masaju kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Tunamshukuru Mheshimiwa George Masaju kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi chake alipokuwa nasi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

SHUGHULI ZA BUNGE

(a) Maswali na Majibu

8. Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkutano huu wa Kumi tunaouhitimisha leo, jumla ya maswali 125 ya msingi na mengine 346 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.

(b) Miswada ya Serikali

9. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Miswada ya Serikali, Bunge lako Tukufu lilipitisha kwa hatua zake zote miswada miwili ya Sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Tisa wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91. Miswada hiyo ni kama ifuatayo: -

(i) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 5) Bill, 2017].

(ii) Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017 [The Public Service Social Security Fund Bill, 2017].

(c) Kamati za Kudumu za Bunge

10. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mkutano huu, Kamati za Kudumu za Bunge zipatazo 16 ziliwasilisha taarifa zake Bungeni. Aidha, taarifa hizo zilisheheni maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa Serikali. Nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wote wa kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia maandalizi ya kazi za kamati hadi kuwasilisha taarifa zao katika Bunge lako tukufu.

11. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea hoja nyingi zilizoibuliwa wakati wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge. Serikali inaamini kuwa hoja hizo zimeibuliwa kwa malengo mazuri ya kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi na uwajibikaji katika sekta ya umma kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora kama ilivyokusudiwa. Serikali inaahidi kuzifanyia kazi hoja hizo hasa wakati huu wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019.

(d) Hoja Binafsi

12. Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkutano huu, Mheshimiwa Suleiman Masoud Nchambi, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, aliwasilisha hoja binafsi kuhusu uzalishaji na ununuzi wa zao la pamba. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa hoja yake hiyo ambayo italeta maboresho katia utendaji wetu.

MAPITIO YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA KIPINDI CHA NUSU MWAKA 2017/2018

13. Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 01 Februari, 2018 Serikali iliwasilisha Bungeni taarifa kuhusu Tathmini ya Hali ya Uchumi na Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia mwezi Julai hadi Desemba, 2017. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kupitia kwa kina taarifa hiyo na kupata picha kamili ya tathmini ya mapitio ya viashiria mbalimbali vya kiuchumi na mwenendo wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 na mwelekeo wake hadi Juni, 2018.

14. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa taarifa hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi na wadau wa maendeleo, napenda kutumia fursa hii kueleza japo kwa uchache kuhusu mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika kipindi cha nusu mwaka na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2017/2018 yanafikiwa.

15. Mheshimiwa Naibu Spika, viashiria mbalimbali vya kiuchumi vinaonesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri. Pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8. Hali hii inaashiria kwamba tuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la mwaka la ukuaji wa asilimia 7.0.

Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huo ni habari na mawasiliano, uchimbaji madini, biashara, ujenzi na uzalishaji viwandani. Mfumuko wa bei uliendelea kutengemaa ambapo ulikuwa wa wastani wa asilimia 4.8 kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2017.

16. Mheshimiwa Naibu Spika, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ilikuwa takriban dola za Marekani bilioni 8.695 ikilinganishwa na wastani wa dola bilioni 8.828 kwa miaka mitatu iliyopita. Aidha, hadi kufikia Novemba 2017, akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 5.91 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa takriban miaka minne kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

17. Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka ni wa kuridhisha ambapo ukusanyaji wa mapato ulifikia shilingi trilioni 12.95 sawa na asilimia 82.8 ya lengo lililopangwa katika kipindi hicho. Matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali za kuhudumia wananchi na miradi ya kipaumbele kama ilivyopitishwa na Bunge lako tukufu.

Miradi hiyo ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge, kugharamia mpango wa elimumsingi bila malipo, kugharamia mpango wa ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, na utekelezaji wa miradi ya usambazaji maji vijijini na mijini. Miradi mingine ni usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA, ununuzi wa meli za abiria na mizigo katika maziwa, ukarabati na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege na kujenga na kuendeleza maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini.

18. Mheshimiwa Naibu Spika, hakika kwa mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na juhudi anazofanya za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kuwa inatekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2017/2018 yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.

Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake. Vilevile, kuwa na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ambao utasaidia kupanua wigo na kudhibiti ukwepaji wa kodi kupitia urasimishaji wa shughuli za uchumi kwa kuwezesha ukuaji wa biashara katika sekta ndogo na za kati ambazo ndiyo mihimili wa kuzalisha ajira na kukuza uchumi.

KILIMO

(a) Hali ya Upatikanaji wa Chakula

19. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/2018, hali ya usalama wa chakula nchini imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula hususan mahindi katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa. Aidha, taarifa zinaonesha kwamba mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi nchini. Ni matarajio yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri.

20. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na usalama wa chakula inaendelea kuwa imara kwa wananchi wote na kwa wakati wote. Hatua hizo ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula kuendelea kusafirisha na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi. Natoa wito kwa wakulima wazitumie vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao stahiki na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.

(b) Hali ya Upatikanaji wa Pembejeo

21. Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima imeimarika. Takwimu zinaonesha kwamba hadi kufikia tarehe 1 Februari, 2018 upatikanaji wa mbolea nchini kwa ajili ya mahindi na tumbaku ulifikia tani 250,376 sawa na asilimia 51.6 ya wastani wa mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka.

Katika kipindi hicho hicho, mbolea za kupandia na kukuzia zenye zipatazo tani 229,839 ziliingizwa nchini na kusambazwa mikoani. Upatikanaji wa dawa za maji na unga (Salfa) kwa ajili ya mazao ya pamba na korosho unaendelea.

22. Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 1 Februari, 2018 upatikanaji wa mbegu bora nchini ulifikia tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji halisi ya tani 60,000 kwa mwaka. Katika kipindi hicho jumla ya tani 22,357 za mbegu bora zilisambazwa nchini.

(c) Usimamizi wa Mazao ya Kimkakati na Kuimarisha Ushirika

23. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nikiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge lako Tukufu tarehe 15 Septemba 2017, nilieleza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kupitia maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha usimamizi utakaokwenda sambamba na uzalishaji na uuzaji wa mazao makuu ya biashara hapa nchini ambayo ni pamoja na pamba, chai, kahawa tumbaku na korosho.

24. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha mnyororo mzima wa kuongeza thamani ya mazao hayo, ili kuhakikisha uwepo wa mfumo madhubuti wa usambazaji mbegu bora, kudhibiti visumbufu vya mimea, upatikanaji wa mbolea kwa wakati, kuboresha mifumo ya masoko pamoja na kufanya tafiti za kina zitakazotatua changamoto za uzalishaji wa mazao hayo.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mazao hayo yanachangia kikamilifu katika uchumi wa nchi na kutumika kama mali ghafi kwenye viwanda. Ili kutimiza malengo hayo, nilipokuwa kwenye ziara zangu katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na mikutano ya wadau wa mazao hayo ya biashara, nilitoa maelekezo mahsusi ikiwemo kuimarisha ushirika, masoko, maafisa kilimo na ugani kutokaa ofisini na kwenda vijijini na mamlaka mbalimbali kufuata taratibu sahihi katika utoaji wa vibali vya ununuzi wa mazao.

25. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa vyama vya ushirika, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu mikataba mibovu ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU). Vilevile, kuchunguza kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu.

26. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeagiza mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) zirudishwe kwenye vyama husika na watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria. Mali za NCU ni pamoja na;

1. Jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd. maarufu kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa wa Station Road;

2. Kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil Mill, kilichopo katika eneo la Igogo;

3. Jengo na viwanja vya Ashock Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.

4. Majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Mkonge na Dengu kilichopo eneo la Igogo, kiwanja namba 41 na 79;

5. Jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo Namba 80, Kitalu “D”;

6. Jengo lililopo katika Kiwanja kilichopo Isamilo Namba 110, Kitalu “D”;

7. Ghala moja katika kiwanja Namba 104, Kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo;

8. Jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja Namba 8 Kitalu “K”;

9. Jengo moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja Namba 24, Kitalu “K”

10. Jengo lililopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”.

27. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa SHIRECU, mali hizo ni ghala la SHIRECU lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya ghorofa tatu (3) iliyopo Kiwanja Namba 1001 “BB” Ilala, Dar es Salaam. Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vilivyo sinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara.

Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba mali tisa za NCU zimepatikana na zimerudi kwenye ushirika huo, wakati mali moja bado iko kwenye hatua ya uchunguzi. Kwa upande wa SHIRECU, mali zote zimepatikana na ziko kwenye hatua ya makabidhiano.

28. Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri wenyewe katika sekta ya kilimo.

Napenda kusisitiza kuwa uendelezaji wa mazao hayo ya kimkakati kwa usimamizi mzuri wa mifumo sahihi ni katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kufikia uchumi wa viwanda.

MIFUGO

Zoezi la Utambuzi wa Mifugo

29. Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 14 Desemba, 2016 tulianza zoezi la upigaji chapa mifugo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo Na. 12 ya mwaka 2010 na kanuni zake za mwaka 2011. Lengo kuu la utambuzi huo ni kudhibiti magonjwa ya mifugo na wizi wa mifugo, kuimarisha usalama wa afya na mazao ya mifugo, kudhibiti usafirishaji na uhamaji wa mifugo kiholela na kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake kitaifa na kimataifa. Pia, utambuzi wa mifugo unasaidia kutambua na kuboresha kosaafu (breed) za mifugo.

30. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ililenga kupiga chapa ng’ombe 17,390,090 kati ya ng’ombe 28,435,825 waliopo nchini. Hadi kufikia tarehe 1 Februari 2018, ng’ombe 15,726,728 sawa na asilimia 90.4 ya lengo la ng’ombe 17,390,090 walikuwa wameshapigwa chapa.

31. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, zoezi la upigaji chapa mifugo linaendelea vizuri na linatarajiwa kukamilika tarehe 30 Machi, 2018. Napenda kusisitiza kwamba zoezi hili la utambuzi wa mifugo ni endelevu na kila ndama anayefikia umri wa miezi sita lazima atambuliwe. Natoa wito kwa wafugaji wote nchini kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Serikali wanaotekeleza zoezi hilo.

VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI

32. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza kaulimbiu ya ujenzi wa viwanda nchini, Serikali imeendelea kuhamasisha utengaji wa maeneo ya uwekezaji sambamba na uendelezaji wa miundombinu wezeshi ili kuvutia wawekezaji katika miradi mbalimbali. Serikali inaendelea kusisitiza kuwa Halmashauri zote ziendelee na mpango wa kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji.

33. Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hiyo, Serikali imeandaa andiko maalum "Blue Print" linaloainisha Sheria, Kanuni na tozo mbalimbali zinazopunguza urahisi wa kufanya biashara nchini. Juhudi nyingine zilizofanyika ni pamoja na taasisi za udhibiti zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuendelea kushirikiana kwa karibu katika utendaji wao na kufanya kazi saa 24 kwa siku 7. Taasisi hizo ni Tume ya Ushindani (FCC), Kituo cha Uwekezaji (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Vipimo Nchini (WMA).

34. Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya upatikanaji rahisi wa huduma za kifedha na mikopo ya gharama nafuu kwa wajasiriamali kupitia Mfuko wa kuendeleza Wajasiriamali Wananchi (NEDF). Katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2017, jumla ya mikopo 1,948 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.344 ilitolewa na kutengeneza ajira 4,438. Katika ajira hizo, wanaume ni 2,130 na wanawake ni 2,308.

35. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaelekeza watendaji wote waliopo katika Mamlaka za Serikali hususan zile za udhibiti na ukusanyaji wa mapato kutotumia vitisho dhidi ya wafanyabiashara wakati wakitekeleza majukumu yao.

NISHATI

Mpango Kamambe wa Upatikanaji wa Nishati

36. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na nishati ya umeme ya kutosha na inayopatikana kwa uhakika. Miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji (Stiegler’s Gorge MW 2,100), Mradi wa Kinyerezi I (MW 180) na Mradi wa Kinyerezi II Extension (MW 240).

37. Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi hiyo ya uzalishaji wa umeme unakwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme ya Makambako-Songea (kV 220) na Singida-Arusha-Namanga (kV 400). Serikali ina matumaini makubwa kwamba mradi wa kusambaza umeme unaokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 900 wa Makambako-Songea (kV 220) utakapo kamilika utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya Wilaya za Songea, Namtumbo, Mbinga, Makambako, Peramiho na Ludewa katika Mikoa ya Ruvuma na Njombe.

REA Awamu ya Tatu

38. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA) ambao umepangwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 ambavyo bado havijapata umeme. Kati ya vijiji hivyo ambavyo havijapata umeme, vijiji 7,697 vimepangwa kupatiwa umeme wa gridi na vijiji 176 pamoja na visiwa vitapatiwa umeme wa nje ya gridi kwa kuwa ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa. Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 689 kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini.

39. Mheshimiwa Naibu Spika, Mipango ya Serikali ya muda mrefu ya kuhakikisha maeneo yenye changamoto kubwa yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika ni pamoja na kutekeleza miradi ya usambazaji umeme ya Somanga-Fungu-Kinyerezi (kV 400), Mtwara-Somanga-Fungu (kV 400) na North West Grid Extension (kV 400).

40. Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa miradi hiyo ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama vile ulipaji fidia, upembuzi yakinifu na tathmini ya athari ya mazingira, kutawezesha Mikoa ya Lindi, Mtwara, Rukwa, Katavi na Kigoma kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo, kuboresha huduma ya umeme katika mikoa hiyo na maeneo mengine nchini. Tayari wakandarasi wapo kila Wilaya kuanza kuweka umeme vijijini.

MADINI

(a) Biashara za Madini ya Tanzanite na Almasi

41. Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba tarehe 06 Septemba, 2017, uliunda Kamati za Bunge kwa ajili ya kuchunguza mwenendo wa mnyororo wa uchimbaji na biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite. Kamati hizo ziliwasilisha taarifa zake zilizoambatana na mapendekezo. Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa mapendekezo hayo kama ifuatavyo: -

Moja: Serikali imekwishaanza majadiliano na wanahisa wa makampuni ya Tanzanite One (T) Limited ili kubaini uwekezaji wao katika kampuni hiyo kwa lengo la kurekebisha mkataba wa umiliki ili uwe kwenye uhalisia;

Mbili: Serikali imehamishia watumishi wake katika mgodi wa Mererani kwa lengo la kusimamia kwa ufanisi shughuli zote za uchimbaji, uzalishaji na uuzaji wa madini ya Tanzanite;

Tatu: Serikali imeboresha utaratibu wa uthamini wa almasi unaofanywa na wataalamu chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania;

Nne: Wajumbe wote wa iliyokuwa Bodi ya Uendeshaji wa Mgodi wa Williamson Diamonds Limited wameondolewa katika nafasi hizo na Serikali inakamilisha taratibu za uteuzi wa wajumbe wapya wa Bodi hiyo; na

Tano: Vilevile, Serikali imeimarisha ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, usafirishaji, uthamini na uuzaji wa madini yote ya vito na almasi nchini.

(b) Ujenzi wa Ukuta Mererani

42. Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 20 Septemba, 2017 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa agizo la ujenzi wa ukuta katika eneo linalozunguka mgodi wa Tanzanite Mererani ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo. Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu pamoja na Watanzania wote kuwa ujenzi wa ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 24.5 upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwezi Aprili, 2018.

(c) Mwenendo wa uwekezaji kupitia wachimbaji wadogo

43. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha uwekezaji katika rasilimali za madini, kupitia wachimbaji wadogo. Aidha, tangu mwaka 2000 hadi kufikia Desemba, 2017 kuna jumla ya leseni hai za uchimbaji mdogo 33,920 kwa nchi nzima. Kati ya hizo, leseni 6,976 zimetolewa kuanzia mwaka 2016/17 hadi hivi sasa. Serikali imetenga maeneo 46 yenye ukubwa wa jumla ya hekta 281,534. Mpango wa Serikali ni kuwekeza katika utafutaji wa madini (mineral exploration) katika maeneo yaliyotengwa ili taarifa ziwasaidie wachimbaji wadogo katika uwekezaji wao.

44. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kusaidia wachimbaji wadogo, natoa wito kwa wachimbaji wote wadogo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji madini kwa ajili ya usalama, afya na utunzaji mazingira. Vilevile, wanapaswa kutekeleza wajibu wao wa kulipa tozo stahiki.

(d) Utatuzi wa migogoro katika maeneo ya machimbo

45. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kutatua migogoro katika maeneo mbalimbali ya machimbo. Miongoni mwa maeneo hayo ni Nyamongo ambako kuna mgogoro kati ya mwekezaji Kampuni ya North Mara na wananchi.

(e) Tume ya Madini

46. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa uundaji wa Tume ya Madini unaendelea. Aidha, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo ameshateuliwa na kikao cha kwanza cha Makamishna wa Tume kilifanyika tarehe 6 Januari, 2018. Kikao hicho pamoja na mambo mengine kilipitia mapendekezo ya uteuzi wa wafanyakazi katika nafasi mbalimbali ndani ya Tume. Hata hivyo, kazi za msingi za Tume kama utoaji wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi (export permit) vinatolewa kwa usimamizi wa Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo.

MIUNDOMBINU

47. Mheshimiwa Naibu Spika, mvua kubwa zilizonyesha kwa kipindi cha mwezi Novemba 2017 hadi Januari 2018, zimeleta athari kubwa kwenye mtandao wa barabara nchini. Kutokana na mvua hizo, hali ya barabara zipatazo 50 katika mikoa 14 ziliathirika ambapo ilikuwa vigumu kupitika kwa urahisi.

48. Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Mikoa ambayo barabara zake ziliathirika na hali ya uwepo wa mvua nyingi ni pamoja na Arusha, Pwani, Dodoma, Dar es Salaam, Iringa, Manyara, Mbeya, Mwanza, Rukwa, Simiyu, Ruvuma, Singida, Songwe na Tabora. Kwa sasa barabara hizo zimefanyiwa matengenezo ya dharura na zinapitika japo si kwa kuridhisha. Aidha, barabara 37 zilizofanyiwa matengenezo zinapitika kwa urahisi.

ELIMU

(a) Mpango Elimumsingi Bila Malipo

49. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza kwa mafanikio Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo kupitia Waraka wa Elimu No. 3 wa mwaka 2016. Waraka huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 sambamba na maelekezo ya Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inayosisitiza utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo.

50. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2017, Serikali imetuma moja kwa moja shuleni jumla ya shilingi bilioni 124.8 kwa ajili ya kutekeleza Mpango huo. Fedha zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za Serikali.

(b) Udhibiti wa Michango Shuleni

51. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku michango ya aina yoyote isiyo ya lazima katika Elimumsingi.

52. Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusu baadhi ya shule kuchangisha michango mbalimbali kutoka kwa wazazi na walezi na kusababisha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kutochangia michango shuleni. Hali hiyo ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na Serikali ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo yamefafanuliwa.

53. Mheshimiwa Naibu Spika, ruhusa ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au taasisi. Hata hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ashirikishe Kamati ya Shule kwa shule za msingi na Bodi za Shule kwa shule za sekondari. Walimu wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma.

(a) Kulinda Mipaka na Viwanja vya Shule

54. Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuwepo kwa changamoto ya umiliki wa ardhi kutokana na baadhi ya shule kutokuwa na hati miliki, Serikali inaendelea kukusanya taarifa kutoka shule mbalimbali za Sekondari kwa lengo la kujua hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo. Hatua hii ya awali inatarajiwa kuhusisha shule za Sekondari Kongwe zipatazo 89.

Zoezi hilo litakapokamilika litawezesha Serikali kuandaa hati miliki kwa shule zenye umiliki wa Serikali na pia kufanya maamuzi kwa shule ambazo umiliki wake uko chini ya taasisi za dini. Aidha, kupitia zoezi hili maeneo ya mipaka ya shule ikiwemo viwanja vya michezo vitatambuliwa na kujumuishwa kwenye ramani za shule. Zoezi la ufuatiliaji wa umiliki wa ardhi kwa shule za msingi na shule za Sekondari zilizobaki za Serikali litaendelea kufanyika ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.

MAJI

(a) Utekelezaji wa Miradi ya Maji Katika Halmashauri

55. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeendelea kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri zote nchini kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza mwaka 2006 hadi 2025. Lengo la programu hii ni kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2020, hali ya huduma ya upatikanaji wa maji inafika asilimia 85 kwa wananchi waishio vijijini na asilimia 95 kwa wale waishio mijini.

56. Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2017, jumla ya shilingi bilioni 55.6 za bajeti ya miradi ya maji kwa mwaka 2017/2018 zilipelekwa katika Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji. Jumla ya miradi 1,466 sawa na asilimia 80.99 ya miradi yote 1,810 iliyopangwa kutekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imekamilika. Miradi iliyobaki ambayo ni 376 na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Aidha, kutokana na changamoto za kuharibika kwa miundombinu ya maji, jumla ya vituo vya kuchotea maji 83,575 kati ya 122,655 vilivyojengwa ndivyo vinavyofanya kazi na vinahudumia wananchi wa vijijini wapatao 20,893,750 sawa na asilimia 56 ya wananchi hao.

57. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Juni, 2020 utekelezaji wa programu hii umelenga kujenga, kukarabati na kuongeza wigo wa miradi ya maji katika vijiji ambapo vijiji 4,105 vitanufaika na mpango huo. Hali kadhalika, vituo vipatavyo 76,334 vya kuchotea maji vyenye uwezo wa kuhudumia watu 19,080,000 vinatarajiwa kujengwa.

(a) Ubadhirifu wa Fedha za Miradi ya Maji

58. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wanaohusika na ubadhirifu wa fedha za miradi ya maji katika Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa. Mathalan, wakati wa ziara yangu ya kikazi katika mkoa wa Mara mwezi Januari, 2018 nilibaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa kwa watendaji wa sekta ya maji mkoani humo. Mapungufu hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maji licha ya Serikali kutuma fedha kila ilipotakiwa kufanya hivyo.

59. Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ubadhirifu huo Serikali imelazimika kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa, ifanye uchunguzi na kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma. Natoa maelekezo kwa Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya wafuatilie utekelezaji wa miradi ya maji iliyopo katika maeneo yao ili wajiridhishe kuwa huduma ya maji safi inapatikana mijini na vijijini.

KUHAMIA DODOMA

60. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza azma yake ya kuhamishia shughuli za Serikali Kuu mjini Dodoma. Aidha, napenda pia kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ofisi yake walihamia rasmi Dodoma tarehe 15 Desemba, 2017 kama ilivyopangwa. Nitumie nafasi hii kumpongeza na kumkaribisha sana Mheshimiwa Makamu wa Rais kwenye Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma.

61. Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kufuatia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Watumishi wa Umma kuhamia Dodoma, jumla ya Watumishi 3,829 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali tayari wamehamia Dodoma. Ujio wao huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma, aliyoyatoa tarehe 23 Julai 2016. Wito wangu kwao ni kwamba watambue wameshafika Dodoma na hatutarajii kuwakuta tena Dar es Salaam.

(a) Mpango wa Kuifanya Dodoma Kuwa ya Kijani

62. Mheshimiwa Naibu Spika, kuhamia kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais mjini Dodoma kumeongeza hamasa ya kuboresha mazingira ya mji huu, hususan baada ya kuzindua rasmi kampeni maalumu ya upandaji miti mjini Dodoma maarufu kama “Kampeni ya Kijanisha Dodoma”.

63. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuifanya Dodoma ambayo ndiyo Makao Makuu ya nchi, kuwa na Ukanda wa Kijani (Green Belt) kupitia mpango huo. Mpango huo unahusisha kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya ukanda wa kijani ambayo ni pamoja na msitu wa Mahomanyika wenye ukubwa wa hekta 2,000, msitu wa Chimwaga Nzuguni wenye ukubwa wa hekta 300 na msitu wa Mbwenzelo wenye ukubwa wa hekta 3,500 pamoja na vilima vya Image na Nyankali.

64. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza malengo hayo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Serikali imeendelea kutoa elimu ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu hususan miti adimu ya asili na makao ya wanyamapori mbalimbali katika kata nane za Ipala, Nzuguni, Kikombo, Ng’ong’ona, Chahwa, Zuzu, Hombolo na Kikuyu Kaskazini. Aidha, kila kata imepewa lengo la kupanda miti isiyopungua 40,000.

65. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa zoezi la upandaji miti, jumla ya miche 34,000 yenye thamani ya Shilingi 34,000,000 imetolewa bure katika kata mbalimbali. Vilevile, kupitia mradi wa TASAF jumla ya miche 138,000 imeoteshwa na inaendelea kusambazwa kwa wananchi. Aidha, kwa sasa Manispaa ya Dodoma inaendelea na Maandalizi ya kuotesha miche mingine ipatayo 200,000 kwa ajili ya msimu ujao.

66. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwashukuru wadau mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bonde la Wami Ruvu, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma wamefanikisha upandaji wa miche 79,000 katika maeneo ya UDOM, Mzakwe, Iseni Park, Nala na Mahomanyika.

67. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu pamoja na kuongeza usimamizi, naziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaandaa miche ya kutosha na kuweka utaratibu wa kila kaya kupanda na kutunza miti isiyopungua mitano. Taarifa za utendaji na maendeleo za Halmashauri zote zioneshe mafanikio yaliyopatikana kutokana na zoezi la upandaji miti. Aidha, utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya utapimwa kutokana na uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.

(b) Uendelezaji wa Makazi na Mpangilio wa Mji wa Dodoma

68. Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo la Serikali la kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma, mahitaji ya viwanja hadi mwezi Februari 2018 yalikuwa viwanja 24,602. Katika kukabiliana na changamoto ya mahitaji ya viwanja, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma hivi sasa inatekeleza mkakati wake wa kuzalisha viwanja 30,000 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Aidha, tayari upimaji wa viwanja vipya 15,316 umekamilika na kazi inaendelea. Viwanja hivi vitaanza kugawiwa kuanzia tarehe 30 Machi 2018. Kiasi kilichobaki cha viwanja 14,684 kitakamilika ifikapo Juni, 2018. Wananchi watauziwa viwanja hivyo kwa bei elekezi itakayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

69. Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wananchi na watumishi wa umma watakaohitaji viwanja wafuate taratibu za maombi ya viwanja pindi vitakapotangazwa rasmi. Zoezi la kubadilisha hati zilizotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kupata HATI MILIKI za miaka 99 linaendelea. Wenye hati za CDA mnasisitizwa kuendelea na taratibu za kuzibadilisha.

HITIMISHO

70. Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda nikushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kutuongoza vema ndani ya Bunge lako tukufu. Vilevile, niwashukuru Wenyeviti wa Bunge ambao kwa umahiri mkubwa wamekuwa wakiendesha vikao vya Bunge hili tukufu. Kadhalika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mbalimbali muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wetu kwa ujumla. Nimshukuru Katibu wa Bunge na wasaidizi wake kwa huduma nzuri na msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia kwa kipindi chote tulichokuwa hapa Bungeni.

71. Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niwashukuru watendaji wa Serikali na taasisi mbalimbali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri na ufanisi mkubwa na hivyo, kufanikisha shughuli zilizopangwa za Bunge lako tukufu bila kuwasahau wanahabari kwa uchambuzi wa hoja na mwenendo mzima wa Bunge na kufikisha habari hizo kwa wananchi. Vilevile, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma ambazo wamekuwa wakizitoa kwa washiriki wa Bunge hili. Pia, niwashukuru madereva wote waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa. Nawatakia kheri kwa safari ya kurejea nyumbani.

72. Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe hoja kwamba Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne tarehe 3 Aprili 2018 saa tatu asubuhi katika ukumbi huu, hapa mjini Dodoma.

73. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday50
mod_vvisit_counterYesterday107
mod_vvisit_counterThis week50
mod_vvisit_counterLast week753
mod_vvisit_counterThis month2960
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days525145
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved