Logo
Saturday, 11 February 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu ahimiza watumishi wafanya mazoezi

*Asema wanatumia akili sana kufikiri, wanakosa muda

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Serikali na wafanyabiashara nchini wajenge tabia ya kufanya mazoezi ili waweze kujikinga na maradhi yanayoepukika.

“Hamasa hii iende zaidi kwa watumishi wa Serikali na wafanyabiashara ambao hutumia akili zaidi kufikiri na wanakaa muda mrefu sana ofisini. Wafanyabiashara nao wanatumia akili sana kufikiri mambo ya biashara na matokeo yake vitambi vinaota,” amesema.

Ametoa wito huo leo asubuhi (Jumamosi, Februari 11, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma walioshiriki matembezi ya hamasa kuanzia viwanja vya Bunge hadi uwanja wa Jamhuri. Siku ya hamasa ya kufanya mazoezi hufanyika Jumamosi ya Pili ya kila mwezi.

Matembezi hayo ambayo yalianzia kwenye viwanja vya Bunge saa 12:25 asubuhi, yaliongozwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alitembea hadi kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere na kisha kupokelewa na Waziri Mkuu ambaye aliendeleza matembezi hayo hadi kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Waziri Mkuu alimshukuru Makamu wa Rais, Mama Samia kwa kuanzisha hamasa hiyo ambayo imewawezesha Watanzania kujumuika kwenye viunga vya michezo na kufanya mazoezi.

“Ukifika uwanjani unaweza kuamua kutembea, kukimbia au kufanya mazoezi ya viungo (physical exercise). Nimefarijika kuona watu wengi wamepokea wito huu kwa makini, hata nikiwa mikoani kwenye ziara za kikazi nimewahi kukuta baadhi ya vikundi vikifanya mazoezi siku ya Jumamosi ya pili ya mwezi,” amesema.

Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kwamba wazee pia wameshiriki mazoezi hayo na kuwataja Balozi mstaafu, Mzee Job Lusinde (miaka 86) na Mzee Mohammed Makbel (miaka 77) kuwa ni miongoni mwa wazee aliowaona kwenye mazoezi hayo.

“Mazoezi yanakufanya ujisikie vizuri na kuondoa virusi vidogo vidogo vya magonjwa kama vile mafua. Mazoezi yanaondoa kabisa maumivu ya misuli na viungo (joints). Lakini pia napenda nisisitize kuwa michezo inajenga urafiki na afya bora,” amesema.

Amesema utaratibu huo wa mazoezi unapaswa kuwa wa hiari na siyo kuwalazimisha watumishi au kuandikisha majina kwa wale wasiofika. “Kikubwa ni kuongeza hamasa ili wafanyakazi washiriki kwa wingi na tutenge viwanja vya mazoezi na bustani za kupumzikia,” amesisitiza.

Amesema ili kuongeza hamasa, matembezi hayo yarudiwe Jumamosi ijayo huku huduma za kupima afya zikipewa uzito katika siku hiyo. “Zoezi la upimaji afya lisiwe la gharama, liwe la bure ili iwe ni kivutio cha watu kushiriki matembezi haya. Hakikisheni watu wanapata fursa ya kupima uzito, damu, shinikizo la damu, kisukari na magonjwa kama hayo,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema kitaalamu inashauriwa mtu afanye mazoezi walau mara tatu kwa wiki kwa muda usiopungua dakika 30.

“Mazoezi ya aina hii yanasaidia mtu kuepuka magonjwa yasiyo ya lazima kama vile saratani, shinikizo la damu na kisukari,” alisema.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bw. Nape Nnauye aliwashukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kuanzisha zoezi hilo la matembezi ambalo alisema limeratibiwa na wizara tatu.

“Zoezi hili litakuwa endelevu. Napenda nikuhakikishie kuwa limeratibiwa na Wizara ya Afya, Wizara ya Habari na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Napenda nisisitize kuwa Halmashauri zitenge maeneo kwenye makazi ya watu ili wananchi wasiende mbali kutafuta viwanja vya michezo pindi wanapotaka kufanya mazoezi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri (OWM – Kazi, Ajira na Vijana) ambaye pia Mbunge wa Dodoma Mjini, Bw. Anthony Mavunde alimuahidi Waziri Mkuu kwamba atashirikiana na uongozi wa mkoa wa Dodoma na wilaya zake kutekeleza maagizo yake ili mkoa huo uwe wa mfano katika suala hilo.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday50
mod_vvisit_counterYesterday107
mod_vvisit_counterThis week50
mod_vvisit_counterLast week753
mod_vvisit_counterThis month2960
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days525145
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved