SERIKALI HAITALIPA MADENI YALIYOKOPWA NA USHIRIKA - MAJALIWA

*Awataka viongozi wa vyama vya ushirika wawe waaminifu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika nchini kutumia vizuri rasimali za vyama hivyo na kwamba Serikali haitalipa deni lolote lililokopwa na vyama hivyo.

“Biashara ya kununua madeni yaliyokopwa na vyama vya ushirika haipo kwenye Serikali hii ya awamu ya tano, badala yake itawachukulia hatua wote waliohusika na ubadhirifu huo.”

Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku wafanyabiashara kuwaibia wakulima kwa kununua kahawa mbichi ikiwa shambani maarufu kama ‘butura’.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Oktoba 6, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara pamoja na wadau wa zao la kahawa baada ya kuwasili mjini Bukoba kwa ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Kagera.

Waziri Mkuu amesema Serikali itachukua hatua kali kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambao si waaminifu na ni wabadhirifu wa mali za ushirika. “Tunahitaji wakulima wapate fedha.”

Amesema Serikali itahakikisha wafanyabiashara wote, hususani wa mazao ya kilimo wanakuwa na mfumo sahihi wa ununuzi wa mazao utakaoongeza tija kwao na kwa wakulima. 

Amesema kwa sasa, Serikali inataka kuondoa mfumo uliopo wa vyama vya ushirika kufanya biashara na badala yake jukumu hilo libakie kwa wafanyabiashara.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara hao waihakikishie Serikali kwamba watanunua kahawa yote iliyopo kwa wakulima pamoja na kwenye vyama vya ushirika. Wafanyabiashara wameridhia kununua kahawa yote.

Awali, Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba alisema katika msimu wa mwaka huu jumla ya kilo 3,000,464 za kahawa isiyokobolewa na kilo 8,191,867 za kahawa safi bado hazijanunuliwa.

Dkt. Tizeba alisema kahawa iliyobakia katika maghala ya vyama vya ushirika ni kama ifuatavyo:- chama cha KCU (1990) kina kilo 1,513,356 za kahawa isiyokobolewa na kilo 1,936,367 za kahawa safi; chama cha KDCU kina kilo 6,012,840 za kahawa safi, Ngara Farmers C.S Ltd kina kilo 592,354 za kahawa isiyokobolewa na kilo 192,660 za kahawa safi.

“Nkwenda AMCOS ina kilo 175,553 za kahawa maganda na kilo 50,000 za kahawa safi na Magata AMCOS kina kilo 433,634 za kahawa safi,” aliongeza.

Alisema vyama vya ushirika vinakabiliwa na changamoto ya kiwango kidogo cha kahawa kinachonunuliwa mnadani na wakati mwingine kutonunuliwa kabisa. Hali hii inatokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia.

Alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa taarifa za upotoshaji kwa wakulima kutoka kwa walanguzi zinazowazuia wakulima kukusanya kahawa yao kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi kwa madai kwamba wao watanunua na kuwapatia bei nzuri.

-ends-