MIRADI YA MAJI KYERWA ITAKAGULIWA NA WAZIRI WA MAJI - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa aende wilayani Kyerwa akakague maendeleo ya miradi ya maji na endapo atabaini ubadhilifu achukue hatua kwa watakaohusika.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 7, 2018) baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Mkewe Mama Mary Majaliwa.

“Waziri wa Maji na Umwagiliaji atakuja hapa na kukakagua miradi yote ya maji inayotekelezwa katika wilaya hii na pale atakapobaini ubadhirifu achukue hatua.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa wananchi wa wilaya hiyo juu ya kutoridhishwa kwao na maendeleo ya miradi ya maji.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini vikiwemo vijiji vya wilaya ya Kyerwa ili kuwawezesha wananchi hasa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo kuliko kutafuta maji.

Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Pia amewataka wananchi hao watunze vyanzo vya maji ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma zote muhimu, hivyo amewataka waendelee kuwa na imani ya Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaboreshea maendeleo katika sekta za afya, maji, elimu, miundombinu na kilimo.

Awali, Mbunge wa jimbo la Kyerwa, Bw. Innocent Bilakwate pamoja na mbunge wa viti maalumu, Bibi Oliver Semuguruka walimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika uboreshwaji wa huduma za maji na afya.

Bw. Bilakwate alisema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tatu katika jimbo hilo, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea, hivyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie.

-ends-